139. Suufiyyah wenye kuonelea kwamba kuna kiwango mtu akifika anatoka katika Shari´ah

Kuna aina mbalimbali za kutoka katika Shari´ah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna sampuli ambazo ni kufuru na aina zengine ni kufuru ndogo. Kuna utokaji wa moja kwa moja na kutoka utokaji wa kisehemu. Wale wanaotoka katika Shari´ah au kitu katika Shari´ah hali ya kuwa wanahalalisha kitendo hicho, ni kufuru. Yule anayetoka hali ya kutokuhalalisha basi huo ni upotevu na sio kufuru.  Wale wanaosema kwamba naadhi ya watu wanaweza kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ambavyo Khidhr alivyotoka katika Shari´ah ya Muusa – wako wenye kuonelea hivo ambao ni katika wale Suufiyyah waliopindukia – ambao wanaona kuwa Suufiy anapofikia daraja fulani ya kumtambua Allaah,  basi anakuwa hana haja ya Mtume kwa sabbau amekwishafika kwa Allaah. Wanasema kuwa Mtume ametumwa kwa watu wasiokuwa na elimu na watu hawa ni wasomi na kwamba wamekwishafika kwa Allaah na wala hawana haja ya Mtume.

Vilevile wanasema kwamba wao wanachukua elimu yao moja kwa moja kutoka kwa Allaah na sisi tunachukua elimu yetu kwa wafu; mfu kutoka kwa mfu mwingine. Wanamaanisha Hadiyth na zile cheni za wapokezi. Ama kuhusu wao wanapokea kwa Allaah. Hivi ndivo wanavosema!

Bali wanasema kwamba ´ibaadah ni zenye kuanguka kwao kwa sababu wamefika kwa Allaah. Matokeo yake hawaswali na wala hawamuabudu Allaah (´Azza wa Jall). Wanaona kuwa ´ibaadah ni za watu wasiokuwa na elimu na watu wa kawaida.  Kadhalika hakuna ambacho kinakuwa haramu kwao. Maamrisho, makatazo, halali na haramu, yote haya ni ya watu wa kawaida ambao hawajafika. Ama wao wamekwishafika na hakuna juu yao halali wala haramu. Wanaona kuwa mambo hayo ni kwa wale wasiokuwa na elimu ambao hawajafika.  Kuhusu wao wamekwishafika na hivyo hakuna juu yao halali wala haramu. Matokeo yake wanahalalisha uzinzi, liwati na mambo mengine ya haramu. Wanaona kuwa hakuna ambacho ni haramu kwao na kwamba wamefika katika mzunguko wa mambo ya wajibu. Uhakika wa mambo ni kwamba ni kama wanavosema kwamba wametoka katika mzunguko wa ´ibaadah na kwenda katika mzunguko wa wendawazimu. Kwa sababu mwenye kufikia kusema hivi basi ni mwendawazimu na hakuna juu yake ´ibaadah. Ama kusema kuwa hana malazimisho kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) kwa sababu eti ameshafika, huku ni kumzulia Allaah (´Azza wa Jall) uongo na kukufuru ujumbe wa Allaah. Hakuna mtu yeyote awezaye kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – pasi na kujali ni kiwango gani cha ´ibaadah, elimu atayofikia na utambuzi wa kumtambua Allaah (´Azza wa Jall). Bali kila wakati elimu yake inapozidi, ´ibaadah zake na utambuzi wake, ndivyo kumtii kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumfuata kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunavyozidi. Hivyo itakuwa ni wajibu kwake kumtii na kumfuata zaidi kuliko wengine. Hii ndio maana ya kauli ya Shaykh:

“Mwenye kudai kwamba kuna yeyote awezaye kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… “

Mwenye kudai hivi amemkufuru Allaah na karitadi kutoka katika dini ya Uislamu. Kwa kuwa atakuwa ameikufuru Qur-aan, Mtume na maafikiano ya waislamu.

Suufiyyah waliopindukia – na ni wingi walioje hii leo – katika vitabu vyao kuna mambo ya ukhurafi, uongo, ujasiri kwa Allaah na Mtume wake kiasi kikubwa. Wanachuooni wamewaraddi na kufichua shubuha na upumbvu. Katika watu madhubuti waliowaraddi ni Shayk-ul-Islaam bin Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn-ul-Qayyim (Rahimahumaa Allaah). Vilevile kundi la wanachuoni wengine wa leo ambao wamewaraddi. Kama mfano wa ´Abdur-Rahmaan al-Wakiyl (Rahimahu Allaah). Ana kitabu kwa jina “Maswraa´-ut-Taswawwuf”.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 180-181
  • Imechapishwa: 07/03/2019