136. Radd juu ya Ahl-ul-Bid´ah katika makhurafi na watu wa matamanio

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah kupitia kwake ameikamilisha Dini. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[1]

MAELEZO

Hakufa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa baada ya Allaah kuikamilisha dini na neema kupitia kwake. Allaah akateremsha juu yake maneno Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”

Aayah hii iliteremka juu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa amesimama ´Arafah katika hija ya kuaga siku ya ijumaa. Baada ya hapo aliishi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kipindi kifupi mpaka alipokwenda kwa Mola Wake aliye juu. Ameuacha Ummah wake katika njia ya wazi kabisa usiku wake ni kama mchana wake na hatopotea kutokamana nayo isipokuwa anayestahiki kuangamia.

Katika Aayah hii kuna ushuhuda kutoka kwa Allaah juu ya ukamilifu wa dini hii na namna inavyoyaenea manufaa ya waja na kuyatatua matatizo na migogoro yao mpaka kisimame Qiyaamah. Ni dini yenye kufanya kazi katika kila zama na mahali. Hawahitajii baada yake Shari´ah nyingine, Kitabu kitachoteremshwa au Mtume mwingine atakayetumilizwa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna jambo utalolipata na wala hakuna kitu kitachozuka isipokuwa katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna ufumbuzi na hukumu yake mpaka siku ya Qiyaamah. Lakini shani ni kwa yule anayeweza kuzichambua na kuzitumia dalili hukuu na qadhiya mbalimbali. Wakipatikana wanachuoni na Mujtahiduun wenye kueneza sharti za Ijtihaad basi Shari´ah hii ni yenye kukamilika na ndani yake kuna ufumbuzi wa matatizo yote. Kasoro inapatikana kwa upande wetu sisi kwa njia ya uchache wa elimu, kutoyafahamu yale aliyoteremsha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) au kuwepo kwa matamanio yanayomgeuza mtu mbali na haki. Vinginevyo dini hii ni yenye kusilihi, yenye kuenea na kamilifu. Allaah ameutosheleza kwao Ummah wa Kiislamu hadi kisimame Qiyaamah pindi itapofanyiwa kazi ipasavo na ikarejelewa katika mambo yake. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.”[2]

Kurejea kwa Allaah ni kurudi katika Kitabu cha Allaah na kurejea kwa Mtume baada ya kufa kwake ni kurudi kwa Sunnah zake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Jambo lolote lile mlilokhitilafiana ndani yake, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[3]

Aayah hii ndani yake kuna Radd juu ya wale wanaituhumu Shari´ah ya Uislamu kwa mapungufu katika wakanamungu, mazanadiki au aina mbalimbali za wale wanaojifanya kuwa ni wanachuoni ambao zimepungua fahamu zao kuzielewa siri za Shari´ah hii. Matokeo yake wakaegemeza mapungufu juu ya Shari´ah na hawakutambua kuwa mapungufu ni kutoka kwao wao. Ndani yake kuna Radd kwa wale wanaotuhumu Shari´ah mapungufu na kwamba haikufumbua haja na manufaa ya waja mpaka siku ya Qiyaamah. Wako wengine wanaosema kuwa inafanya kazi katika zile zama za mwanzo. Kwa sababu wajinga wengi wanapoambiwa jambo fulani ni hukumu ya Kishari´ah wanasema kuwa hizo ni zama za Mtume na kwamba ni zama za mwanzo na kwamba hii leo hali na mambo yamebadilika na kwamba hukumu za Kishari´ah ni juu ya watu waliopita na ni juu ya matatizo yaliyokwisha. Hivi ndivo wanavosema, jambo ambalo ni kufuru na ni kuyakadhibisha maneno Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

”Leo nimekukamilishieni dini yenu.”

Allaah ameikamilisha dini juu ya Ummah huu mpaka kisimame Qiyaamah juu ya kila zama, kila mahali na kila kizazi katika watu. Jengine ni kwamba ndani yake kuna Radd kwa watu wa Bid´ah ambao wanazua ´ibaadah kutoka vichwani mwao na wanazinasibisha na dini ilihali hazina dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Wamezua kwa kuonelea kuwa ni mazuri au kwa kuwafuata kibubusa wale wenye kuwajengea dhana nzuri katika makhurafi, watu wenye tamaa na matamanio. Matokeo yake wanateremsha ndani ya dini ´ibaadah ambazo hazikuteremsha Allaah.

[1] 05:03

[2] 04:59

[3] 42:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 271-274
  • Imechapishwa: 15/02/2021