135. Kwenda katika tanzia kukiwa na Bid´ah

Swali 135: Je, inafaa kwenda katika tanzia ya maiti ikiwa kuna Bid´ah kama mfano wa kisomo cha Qur-aan pamoja na kunyanyuwa viganja vya mikono kabla ya kutoa salamu[1]?

Jibu: Sunnah ni kuwatembelea wafiwa wa maiti kwa ajili ya kuwapa pole. Ikiwa kuna maovu basi akawakataze na awabainishie. Hivyo yule mgeni anakuwa amekusanya kati ya manufaa mawili; anawapa pole na anawakemea pamoja na kuwanasihi.

Ama kitendo cha kusoma Qur-aan peke yake hakuna neno. Wakikusanyika na mmoja wao akasoma Qur-aan mbele ya mkusanyiko wao, kama mfano wa kusoma al-Faatihah na nyenginezo, ni sawa na katika jambo hilo hakuna maovu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anakusanyika pamoja na Maswahabah zake basi kunasomwa Qur-aan. Wakikusanyika katika kikao chao cha tanzia na mmoja wao au baadhi yao wakasoma sehemu ya Qur-aan basi ni kheri kuliko kukaa kwao kimya.

Lakini ikiwa kuna Bid´ah mbali na hii, kama vile wafiwa wa maiti kuwatengenezea chakula watu, basi wafundishwe na wanasihiwe kuacha jambo hilo. Yule mfariji akiona maovu basi anatakiwa kutoa nasaha. Amesema (´Azza wa Jall):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖوَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidiane katika wema na kumcha Allaah na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.”[2]

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayakemee kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa ulimi wake. Asipoweza, basi afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[4]

Kuhusu maneno ya muulizaji pale aliposema kuwa mtoa pole hunyanyua mikono yake na akasoma Qur-aan kabla ya kuingia ndani na kabla ya kutoa salamu, hii ni Bid´ah na haina msingi. Lakini ni sawa ikiwa mmoja katika wao atawasomea wote Qur-aan kwa ajili ya faida.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/371-372).

[2] 05:02

[3] 05:02

[4] Ahmad (10766) na Muslim (49).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 97-98
  • Imechapishwa: 18/01/2022