134. Kitenguzi cha tisa: Mwenye kuitakidi kwamba baadhi ya watu wanaweza kutoka katika Shari´ah ya Muhammad

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La tisa:

Mwenye kuitakidi ya kwamba baadhi ya watu wana haki ya kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama jinsi Khidhr alivyopata kutoka katika Shari´ah ya Muusa (´alayhis-Salaam), amekufuru.

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

”Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitokubaliwa kutoka kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (Aal ´Imraan 03 : 85)

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

”Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.” (al-A´raaf 07:158)

MAELEZO

Ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) kamtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wote; waarabu na wasiokuwa waarabu, waliopewa Kitabu, ambao hawakupewa Kitabu na wengineo bali mpaka majini. Kawajibisha juu ya viumbe wote, majini na watu, kumfuata Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ni sifa maalum kwake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mitume walikuwa wakitumwa kwa watu wao maalum. Mimi nimetumwa kwa watu wote.”[1]

Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا

”Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote hali ya kuwa ni mbashiriaji na muonyaji.” (Sabaa´ 34:28)

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

”Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote ambaye pekee Yake anao ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu wa haki  isipokuwa Yeye, Anahuisha na Anafisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, Mtume asiyejua kusoma wala kuandika, ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake na mfuateni ili mpate kuongoka.” (al-A´raaf 07:158)

Amesema kuhusu mayahudi na manaswara:

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Wale ambao wamemfuata Mtume, Nabii asiyejua kusoma wala kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza maovu na anawahalalishia mazuri na anawaharamishia maovu na anawaondoshea mazito yao na minyororo [Shari’ah ngumu] zilizokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafuata Nuru ambayo imeteremshwa pamoja naye, basi hao ndio wenye kufaulu.” (al-A´raaf 07:157)

Hivyo kawajibisha juu ya mayahudi na manaswara kumfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumnusuru na kumtukuza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatosikia yeyote kuhusu mimi, si myahudi wala mnaswara, kisha asiamini yale niliyokuja nayo isipokuwa ataingia Motoni.”

Aliona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mkononi mwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kukiwa kuna makaratasi ya Tawraat ambapo akakemea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitendo hicho na akamwambia:

“Je, una mashaka, ee mwana wa al-Khattwaab? Lau ndugu yangu Muusa angelikuwa hai asingelifanya jengine isipokuwa kunifuata.” Akasema ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh): “Tumemridhia Allaah kuwa nditye Mola wetu, Uislamu kuwa dini ndio yetu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ndiye Nabii na Mtume wetu.”[2]

Allaah (´Azza wa Jall) alichukua ahadi kwa Mitume ya kwamba atapotumwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mmoja wao akawa yuko hai basi amfuate. Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ النَّبِيِّينَ لَمَا آتَيْتُكُم مِّن كِتَابٍ وَحِكْمَةٍ ثُمَّ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مُّصَدِّقٌ لِّمَا مَعَكُمْ لَتُؤْمِنُنَّ بِهِ وَلَتَنصُرُنَّهُ ۚ قَالَ أَأَقْرَرْتُمْ وَأَخَذْتُمْ عَلَىٰ ذَٰلِكُمْ إِصْرِي ۖ قَالُوا أَقْرَرْنَا ۚ قَالَ فَاشْهَدُوا وَأَنَا مَعَكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ فَمَن تَوَلَّىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَأَفَغَيْرَ دِينِ اللَّـهِ يَبْغُونَ وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ

“Pindi Allaah alipochukua fungamano kwa Manabii [akawaambia] “Kwa niliyokupeni kutoka Kitabu na hekima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha yaliyo pamoja nanyi, [akawaambia basi] ni juu yenu kumwamini na kumnusuru.” Akasema: “Je, mmekiri na mmekubali kuchukua juu ya hayo agizo Langu?” Wakasema: “Tumekiri”. Akasema: “Basi shuhudieni na Mimi niko pamoja nanyi katika wenye kushuhudia.” Basi atakayekengeuka baada ya hayo, basi hao ni mafasiki. Je, wanataka dini isiyokuwa ya Allaah na hali Kwake amejisalimisha kila aliye katika mbingu na katika ardhi akipenda asipende na Kwake watarejeshwa.” (Aal ´Imraan 03:81-83)

Dalili juu ya hili ziko wazi.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (335) na Muslim (521).

[2] Ameipokea Ahmad (15156), Ibn Abiy ´Aaswim (50), ´Abdur-Razzaaq katika “al-Muswannaf” (10164) na ´Abdul-Barr katika “al-Jaamiy´” (1497).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 175-177
  • Imechapishwa: 05/03/2019