131. Hijrah na lengo la kusoma historia ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hijrah ni kutoka katika mji wa kikafiri na kwenda katika mji wa Kiislamu. 

MAELEZO

Maana ya kuhama kiliugha ni kukiacha kitu.

Kuhusu maana ya kuhama Kishari´ah, ni kama alivyoelezea Shaykh, ni kutoka katika mji wa kikafiri na kwenda katika mji wa Kiislamu. Huku ndio kuhama kwa Kishari´ah. Kuhama ni kitendo kitukufu ambacho Allaah amekiambatanisha na jihaad katika Aayah nyingi.

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipohama kwenda Madiynah Muhaajiruun ambao walikuwa Uhabeshi walirudi Madiynah na wakakusanyika Madiynah na himdi zote zinamstahikia Allaah. Waislamu katika Muhaajiruun na Answaar Madiynah wakajenga dola na yule alikuwa anasilimu basi anaenda kwao. Hapo ndipo Allaah aliweka Shari´ah nyenginezo za dini. Akafaradhisha juu ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swawm na zakaah katika mwaka wa pili baada ya kuhajiri. Pia akafaradhishiwa hajj katika mwaka wa pili baada ya kuhajiri kutokana na maoni yenye nguvu. Hapo ndipo nguzo za Uislamu zikakamilika. Ya kwanza yake ni shahaadah na ya mwisho yake ni kuhiji katika nyumba tukufu ya Allaah.

Kwa kufupiza haya ni kwamba tunatakiwa kujua kuwa Tawhiyd ndio jukumu la kwanza wakati wa kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba mlinganizi anatakiwa kuanza kwayo kabla ya kuanza kwa swalah, swawm, zakaah na hajj. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibaki miaka kumi akilingania katika Tawhiyd na akikataza shirki. Hayo yalikuwa kabla ya kuamrishwa swalah, zakaah, hajj wala kufunga. Faradhi hizi zilifaradhishwa kwake baada ya kuthibiti kwanza Tawhiyd.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati anapowatuma walinganizi alikuwa kwanza akiwaamrisha wawaite watu katika Tawhiyd. Hayo unaweza kuyaona katika Hadiyth ya Mu´aadh:

“Hakika wewe unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab. Hivyo basi, iwe jambo la kwanza utalowalingania kwalo ni ´kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah`. Wakikuitikia jambo hilo, basi wafundishe kwamba Allaah amefaradhisha juu yao swalah vipindi vitano… “[1]

Hayo yamejulisha kwamba hakuamrishwi swalah, zakaah wala swawm isipokuwa baada ya kuihahakikisha Tawhiyd na kupatikana Tawhiyd na kwamba yule mwenye kuanza kwa isiyokuwa Tawhiyd basi Da´wah yake ni isiyokuwa na mafanikio yoyote na mfumo wake ni wenye kwenda kinyume na mfumo wa Mitume wote (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mitume wote kitu cha kwanza walichokuwa wakianza nacho ni Tawhiyd na kuitengeneza ´Aqiydah. Huu ni mfumo ambao wapitaji wanatakiwa kuutambua. Kwa sababu hii leo wamekuwa wengi wenye kuudharau mfumo huu na matokeo yake wanaugeuza mfumo huu na hivyo wanajichagulia wao wenyewe mfumo kutoka vichwani mwao na kutoka vichwani mwa wajinga wengineo. Ni lazima kurejea kwenye mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio faida ya kumjua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), historia yake na kulifanya jambo hilo kuwa ni msingi wa tatu. Unapaswa kujua ni vipi aliwalingania watu na ni upi mfumo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kulingania mpaka uweze kuufuata. Kwani yeye ndiye kiigizo chema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (1395) na Muslim (19).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 264-266
  • Imechapishwa: 10/02/2021