130. Kuhajiri kwa Mtume pamoja na Abu Bakr kuelekea Madiynah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada yake akaamrishwa kufanya Hijrah kwenda al-Madiynah.

MAELEZO

Baada yake akaamrishwa… – Wakati kero, shari za Quraysh za kuzuia watu kutokamana na njia ya Allaah, kuwatia dhiki waislamu kulipozidi na kuwaadhibu wale waislamu wanyonge wasiokuwa na kikundi cha watu cha kuwalinda ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akawapa idhini kuhama kwenda Uhabeshi na kufanya Hijrah ya kwanza. Kwa sababu alikuweko mfalme ambaye hadhulumiwi yeyote mbele yake. Mfalme huyo alikuwa mkristo lakini hata hivyo alikuwa mwadilifu. Walihama kutoka kwao watu wengi. Pindi Quraysh walipojua kuhusu kuhama kwao kwenda Uhabeshi waliwaagiza wajumbe wawili kuwafuata ambapo mmoja wao alikuwa ni ´Amr bin al-Aasw na walikuwa wamebeba zawadi kwa ajili ya an-Najaash na wakamwambia kwamba watu wale ni jamaa zao, wanataka kuwarudisha nyuma, kwamba ni watu waovu, kwamba wataeneza ufisadi nchini na tuhumu zengine nyingi. Wakampa zawadi walizokuwa nazo ili wamghuri. Lakini yeye (Rahimahu Allaah) aliwaita wahamiaji wale ili awasikilize na akawapa khiyari ya kubaki Uhabeshi. Wajumbe wawili wale wakarudi wakiwa ni wenye kukata tamaa na wakawa wamebaki wenye kubaki huko Uhabeshi katika wale wahamiaji. Kisha Allaah akamneemesha an-Najaash ambapo akaingia katika Uislamu na akaufanya vizuri Uislamu wake. Wakati alipokufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye pamoja na Maswahabah zake wakamswalia swalah ya ghaibu. Hivyo ikawa kwa Hijrah yao kwake kuna kheri juu yake ambapo Allaah alimwongoza kwa sababu yao na akaingia ndani ya Uislamu.

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakutana na kundi la Answaar Minaa katika msimu wa hajj. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiidhihirisha nafsi yake kwa makabila katika msimu wa hajj. Akienda kwenye mashukio ya waarabu Minaa na akiwalingania katika dini ya Allaah. Siku moja akabahatikiwa kukutana na watu katika Answaar ambapo akawalingania katika dini ya Allaah ambapo akawaonyesha yale alionayo. Wakakubali kutoka kwa Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulinganizi wake na wakampa kiapo cha usikivu juu ya Uislamu na wakarejea kwa watu wao kutoka katika msimu wa hajj na wakawalingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Wakajaa katika msimu uliokuja baada yake watu wengi zaidi kuliko wale waliokuwa katika msimu wa kwanza. Walikuja watu wa Answaar na wakampa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kiapo cha usikivu. Hiyo ilikuwa ni bay´ah ya ´Aqabah ya pili. Walimpa kiapo cha usikivu juu ya Uislamu, kwamba watamnusuru akihamia kwao na kwamba watamlinda kwa yale wanayozilinda nafsi zao wao wenyewe na watoto wao. Kipindi hicho au kwa msemo mwingine baada ya kiapo hicho kilichobarikiwa ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha wale waislamu waliokuwa Makkah wahame kwenda Madiynah. Wakahama waliohama kwenda Madiynah. Akabaki Mtume na baadhi ya Maswahabah zake. Kisha Mtume wa Allaah akampa idhini Mtume Wake kuhajiri.

Wakati Quraysh walipojua kuhusu kuhajiri kwa Maswahabah kwenda Madiynah na wakajua kuhusu kiapo kilichotokea kati yake yeye na Answaar wakaogopa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asije kukutana na Maswahabah zake huko Madiynah, wakajenga nguvu na wakawa na kinga. Katika usiku huu ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitaka kuanza kuhajiri wakaja na kuizingira nyumba yake na wakasimama mlangoni wakiwa wamebeba silaha zao wanachotaka ni kumuua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah akamweleza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha ´Aliy kulala kwenye kitanda chake ili washirikina wamuone na wafikirie kuwa ndiye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) akalala kwenye kitanda cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akajifunika shuka ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Washirikina wakawa wanamsubiri atoke wakidhani kuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatoka kati yao pasi na wao kuhisi. Allaah aliwapofoa macho yao kutokamana naye na akachukua mchanga na kuwamiminia juu ya vichwa vyao. Akatoka kupita kati yao na akaenda kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Wakatoka na kwenda katika pango la Thawr na wakajificha ndani yake kwa muda wa siku tatu. Quraysh waliwataka watu kumtafuta kwa njia yoyote ile. Ni mamoja wamempata akiwa hai au maiti. Wakati walipokata tamaa ya kumpata baada ya kumtafuta kwa marefu na mapana waliahidi malipo kwa ambaye atamleta (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa hai au maiti. Wakati walipokata tamaa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Swahabah wake walitoka pangoni wakapanda vipando na wakasafiri kwenda Madiynah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 261-264
  • Imechapishwa: 10/02/2021