18- Inajuzu kwao kufunua uso wa maiti na kumbusu na kumlilia kwa muda wa siku tatu. Kutokana na hilo kumepokelewa Hadiyth zifuatazo:

Ya kwanza: Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwa kusema:

“Wakati alipouawa baba yangu nilikuwa ni mwenye kumfunua nguo kutoka usoni mwake na nikilia. Watu wakinikataza na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hanikatazi. [Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha kuinuliwa]. Shangazi yangu Faatwimah akawa analia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Lia au usilie. Malaika hawakuacha kumfunika kwa mbawa zao mpaka mlipomyanyua.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim, an-Nasaa´iy, al-Bayhaqiy, Ahmad (03/298). Ziada ni ya Muslim na an-Nasaa´iy.

Ya pili: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) alikuja akiwa juu ya farasi wake kutoka nyumbani mwake [sehemu hiyo] mpaka aliposhuka na akaingia msikitini. [´Umar alikuwa akiwazungumzisha watu] hakuwazungumzisha watu mpaka alipoingia kwanza ndani kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Akamkusudia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali amefunikwa kwa shuka ya kiyemeni yenye michilizimichilizi ambapo akamfunua uso wake kisha akamuinamia na akambusu [kati ya macho yake]. Halafu akalia na akasema: “Namtoa fidia baba yangu na mama yangu kwa ajili yako Nabii wa Allaah. Allaah hatokukusanyia kifo mara mbili. Kuhusu kifo ambacho tayari ulimo tayari kimeshapita.

Katika upokezi mwingine:

“Hakika umeshakufa kifo ambacho hutokufa tena baada yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/89) na an-Nasaa´iy (01/260-261). Ziada ni yake katika upokezi moja wapo. Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (2155), al-Bayhaqiy (03/406) na wengineo.

Ya tatu: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia nyumbani kwa ´Uthmaan bin Madh´uun akiwa ameshakufa ambapo akamfunua uso wake akamuinamia na kumbusu mpaka nikaona machozi yakitiririka kwenye mashavu yake.”

Ameipokea at-Tirmidhiy (02/135), al-Bayhaqiy ameisahihisha na wengineo. Ina ushahidi kwa cheni ya wapokezi nzuri. Rejea katika “Majma´ az-Zawaaid” (03/20). Kisha ikabainika kwamba ndani yake kuna udhaifu miwili. Kashf-ul-Astaar” (01/383). Nimeitaja katika “adh-Dhwa´iyfah” (6010).

Ya nne: Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwa kusema:

“Tuliingia pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Abu Sayf – alikuwa ni mume wa yule mama aliyekuwa akimnyonyesha mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); Ibraahiym. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamchukua Ibraahiym, akambusu na akamshumu. Kisha baada ya tukio hilo tukaingia tena kwake na Ibraahiym alikuwa katika hali ya kukata roho. Macho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yakawa yanatiririkwa na machozi. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf akasema: “Wewe pia, ee Mtume wa Allaah?” Akajibu: “Ee mwana wa Ibn ´Awf! Hakika si vinginevyo ni huruma kisha akalifuatilizia chozi lile chozi lingine. Akasema: “Hakika macho hutokwa na machozi na moyo unahuzunika. Na hakika hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola Wetu. Ee Ibraahiym! Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/35), Muslim na al-Bayhaqiy (04/69) amepokea mfano wake.

Ya tano: ´Abdullaah bin Ja´far (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapa muhula familia ya Ja´far siku tatu kutowaendea. Kisha baada ya hapo akawaendea na kusema: “Msimlilie tena ndugu yangu baada ya leo… “

Ameipokea Abu Daawuud (02/124), an-Nasaa´iy (02/292) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Ameipokea pia Ahmad kwa ukamilifu zaidi. Tamko lake litakuja katika “taazia” – Allaah (Ta´ala) akitaka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 30/12/2019