13. Udhuru wa kuswali nyumbani kwa ambaye ana harufu ya kukera watu msikitini?

Swali 13: Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh makatazo ya kukaribia msikiti kwa ambaye amekula vitunguu maji, vitunguu saumu au figili. Je, kunaingia vilevile vile vitu vyenye harufu ya kukera – isitoshe ambavyo ni haramu – kama mfano wa sigara? Je, hiyo ina maana kwamba atakayetumia vitu hivi basi anapewa udhuru wa kukosa swalah ya mkusanyiko kwa njia ya kwamba hapati dhambi kwa kukosa kwake[1]?

Jibu: Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Atakayekula kitunguu maji au kitunguu saumu basi asisogelee msikiti wetu na aswali nyumbani kwake.”[2]

“Hakika Malaika wanakereka kwa yale yanayowakera watu.”[3]

Vilevile kila ambacho kina harufu ya kukera kama kitunguu maji na kitunguu saumu basi kina hukumu moja kama kitunguu maji na kitunguu saumu kama vile mvutaji sigara, ambaye ananuka kikwapa au wengineo basi kumechukizwa kwao kuswali pamoja na mkusanyiko. Amekatazwa kufanya hivo mpaka atumie vinavyoondosha harufu hii. Kama anaweza ni lazima kwake kufanya hivo ili apate kutekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia ambayo ni kuswali katika mkusanyiko.

Kuhusu kuvuta sigara ni haramu kwa hali zote. Ni lazima kwake kuiacha katika nyakati zote. Istoshe ina madhara makubwa katika dini, dunia na mali.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/83-84).

[2] al-Bukhaariy (808) na Muslim (875-876).

[3] Ahmad (14483) na Muslim (874).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 26/11/2021