Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

05 – Mwenye kuchukia kitu katika yale mambo aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hata kama atakifanya, basi anakufuru.

MAELEZO

Ambaye anachukia kitu miongoni mwa yale mambo aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hata kama atakifanya, anakufuru. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekuja na Shari´ah ya swalah. Yule mwenye kuchukia swalah amekufuru. Vilevile amekuja na Shari´ah ya zakaah na kadhalika. Kwa hivyo mwenye kuchukia kitu alichokuja nacho Mtume wa Allaah, hata kama atakifanyia kazi, basi amekufuru. Vivyo hivyo amekuja na Shari´ah ya kuoa wake wengi. Yule mwenye kuchukia hukumu hii ya Kishari´ah ambayo ni kuoa wake wengi, basi amekufuru.

Kwa ajili hii inawapaswa wanawake wafahamu kuwa haiwastahikii wao kuchukia kuoa wake wengi. Hii ni hukumu ya Allaah na Mtume Wake. Lakini hata hivyo ikiwa anachukia jambo hili na halipendi na akawa na chuki ya kimaumbile – na si kwamba anaichukia ile hukumu ya Kishari´ah – hilo halimdhuru. Au akachukia kwa vile baadhi ya wanaume hawafanyi uadilifu. Kwa msemo mwingine ni kwamba akawa ni mwenye kuchukia kuolelewa juu yake kwa sababu anachelea mwanaume huyu hatofanya uadilifu haina neno. Ama ikiwa anachukia ile hukumu ya Kishari´ah, ambayo ni kuoa wake wengi, huku ni kuritadi. Kwa msemo mwingine ikiwa anachukia chuki ambayo ni ya kubughudhi yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili ya hili ni maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

“Hivyo kwa kuwa wao wameyachukia yale aliyoyateremsha Allaah, basi akayaporomosha matendo yao.”[1]

Yule mwenye kuchukia au kubughudhi kitu chochote katika yale aliyoteremsha Allaah au yaliyoweka Allaah na Mtume Wake katika Shari´ah, basi anakuwa kafiri:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Haiwi kwa muumini mwanamme na wala kwa muumini mwanamke pindi Allaah anapohukumu na Mtume Wake jambo lolote iwe wana khiyari katika jambo lao – na yule anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi kwa hakika amepotoka upotofu wa wazi.”[2]

Akichukia uwekwaji wa Shari´ah ya swalah, zakaah, swawm, hajj au uoaji wa wake wengi – ni mamoja awe analichukia au kulibughudhi – anakuwa kafiri. Kwa sababu kitendo hicho kinapingana na imani. Kumpenda Allaah na Mtume Wake ni jambo la lazima. Asiyempenda Allaah na Mtume Wake ni kafiri. Ukamilifu wa mapenzi ni kutanguliza mapenzi ya kumpenda Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kila kitu. Lakini ule msingi wa mapenzi ni lazima uwepo. Asiyempenda Allaah na Mtume Wake ni kafiri.

Kwa kifupi ni kwamba yule mwenye kuchukia au kubughudhi kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au katika yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah katika Kitabu Chake, akamchukia Allaah au akamchukia Mtume Wake, basi anakuwa ni kafiri na mwenye kuritadi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

“Hivyo kwa kuwa wao wameyachukia yale aliyoyateremsha Allaah, basi akayaporomosha matendo yao.”

Jengine ni kwa sababu chuki hii inapingana na imani. Aidha mapenzi ya kumpenda Allaah na Mtume Wake ndio msingi wa imani. Hivyo basi asiyempenda Allaah na Mtume Wake ni kafiri. Mwenye kubughudhi au kuchukia kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inapelekea kutompenda Allaah na Mtume Wake, jambo ambalo ni ukafiri na kuritadi. Tunamuomba Allaah usalama.

[1] 47:09

[2] 33:36

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 15/04/2023