13. Shaam ndio sehemu ya mwisho ardhini

86- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Mimi nasoma katika kitabu cha Allaah ya kwamba ardhi itaharibika miaka arubaini kabla ya Shaam.”

87- Tubayy´ amesema:

“Ardhi itaharibika na Shaam itaota mauwa. Wakazi wake watakuwa kama katika mkomamanga. Hakutobaki sehemu ardhini wala mlimani isipokuwa wataishi watu. Miti ambayo hata haikukuwa wakati wa Nuuh itakuwa. Kasiri zilizo ndefu kabisa zitajengwa. Utapoyaona hayo basi ujue kuwa muda wako umefika.”

88- Bahiyr bin Sa´d amesema:

“Shaam itabaki baada ya kuharibika kwa ardhi miaka arubaini.”

89- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Shaam kutajengwa msikiti ambao utabaki miaka arubaini baada ya ardhi kuharibika.”

Haafidhw Abul-Qaasim amesema:

“Haya ndio sahihi zaidi. Kumepokelewa kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw kinyume na hayo ikiwa ni pamoja na:

90- Abu Ja´far bin Muhammad bin ´Uthmaan bin Abiy Shaybah amesema: Baba yangu ametuhadithia: Mu´aawiyah bin Hishaam ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia kutoka kwa Huswayn, kutoka kwa Abu Dhwabyaan, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw ambaye amesema:

“Kitu cha kwanza kitachoharibiwa ardhini ni Shaam.”

Abu Ja´far ametiliwa dosari. Kadhalika dalili zinatilia nguvu yale maoni ya kwanza, kama alivyosema Abul-Qaasim. Shaam itabaki ni yenye kuishi ndani yake watu baada ya al-Madiynah kuharibika, kujitokeza ad-Dajjaal, kushuka kwa ´Iysaa bin Maryam, kutoka kwa Ya´uuj na Ma´juuj na baada ya kujitokeza kwa moto ambao ndio alama ya kwanza ya Qiyaamah. Baada ya hapo Allaah atatuma upepo mzuri ambao utazichukua roho za waumini. Yote haya yametajwa katika Hadiyth mbalimbali.

91- Muslim amepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“ad-Dajjaal atajitokeza katika Ummah wangu na atabaki arubaini – sijui kama ni siku arubaini, miezi au miaka. Allaah amtume ´Iysaa bin Maryam kama vile ni ´Urwah bin Mas´uud. Amtafute na amuue. Baada ya hapo aishi kati ya watu miaka saba. Kisha Allaah atume upepo wenye baridi kutokea Shaam na kusibaki juu ya ardhi yeyote ambaye moyoni mwake kuna punje ya wema – bi maana imani – isipokuwa utamchukua. Hata kama mmoja wenu ataingia ndani ya mlima utamwingilia na kuchukua uhai wake.”

Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Viumbe waovu watabaki wakiwa na uzito wa ndege na thamani za wanyama wa pori. Hawatambui wema na wala hawakatazi maovu. Shaytwaan atajionyesha kwao na kuwaambia: “Je, hamniitikii?” Waseme: “Unatuamrisha nini?” Atawaamrisha waabudu mizimu. Watakuwa na maisha mazuri. Baada ya hapo litapulizwa parapanda… “

Hakutobaki muumini isipokuwa atajiunga na ´Iysaa bin Maryam njiani kuelekea Twuur. Maji yote yatatoweka isipokuwa ya Shaam. Maji ya dunia nzima yatatoka Shaam na huko ndiko yatakorudi.

92- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake. Hakuna maji yoyote matamu yananywiwa isipokuwa yanatoka katika mlima huu. Hata chemchem ya bahari inatoka katika mlima huu.”

93- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Radi na umeme vinakaribia kuhamia kwenda Shaam mpaka visiwepo isipokuwa kati ya Eufrat na al-´Ariysh.”

94- al-Awzaa´iy amesema:

“Radi na umeme vitahajiri sehemu ya Ibraahiym mpaka kusibaki tonye hata limoja la maji isipokuwa kati ya Eufrat na al-´Ariysh.”

95- Abu Qulaabah amesema:

“Radi na umeme vitahajiri kutoka Iraq na kwenda Shaam mpaka huko kusiwepo radi na umeme zaidi.”

Yanayothibitisha kuwa Shaam ndio sehemu ya mwisho ni moto ambao ndio alama ya kwanza ya Qiyaamah. Utawafukuza watu kuelekea Shaam.

96- Imaam Ahmad, at-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kutajitokeza moto Hadhramawt ambao utawafukuza watu.” Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha nini?” Akasema: “Shikamaneni na Shaam.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

97- Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa Bahz bin Hakiym ambaye ameeleza ya kwamba alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha wapi?” Akasema: “Hapa!” Akaashiria Shaam kwa mkono wake na kusema: “Hakika nyinyi mtakusanywa kwa miguu na kwa kupanda kipando na mtaachwa juu ya nyuso zenu.”

Katika upokezi wa Imaam Ahmad imekuja:

“Akaashiria Shaam kwa mkono wake na kusema: “Pale ndipo mtakusanywa.”

Ameisahihisha vilevile at-Tirmidhiy.

98- al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Anas ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Alama ya kwanza ya Qiyaamah ni moto utaojitokeza mashariki na kuwakusanya magharibi.”[1]

Magharibi ni Shaam na Allaah ndiye anajua zaidi.

99- Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Dharr aliyesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafanya nini ukifukuzwa kutoka al-Madiynah?” Nikasema: “Basi nitaishi kwa raha na amani na kwenda zangu na kuwa njiwa katika njiwa za Makkah.” Ndipo akasema: “Utafanya nini ukifukuzwa kutoka Makkah?” Nikasema: “Basi nitaishi kwa raha na amani na kwenda zangu Shaam na ardhi Takatifu.” Akasema: “Utafanya nini ukifukuzwa kutoka Shaam?” Nikasema: “Ninaapa kwa Yule aliyekutuma kwa haki ya kwamba nitauweka upanga wangu juu ya bega langu.” Akasema: “Au kilicho bora kuliko hicho? Sikiliza na utii hata kama atakuwa mja wa kihabeshi.”

[1] al-Bukhaariy (3938).

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 99-112
  • Imechapishwa: 10/02/2017