13. Ni nani anayefaidika na kumwabudu Allaah?

Kisha Allaah (Jalla wa ´Alaa) akasema:

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ

“Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala sitaki wanilishe.”[1]

Hapa kuna ubainifu ya kwamba Allaah hana haja ya ´ibaadah zao; wao ndio wenye kuhitajia kumwabudu Allaah. Allaah amewaumba majini na watu ili wamwabudu Yeye. Lakini hata hivyo si mwenye kuwahitajia. Kwa hiyo ni nani mwenye kuhitajia ´ibaadah? Ni waja wao wenyewe. Kwa ajili hii ndio maana akasema (Ta´ala):

وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ

“Muusa  akasema: “Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah ni mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[2]

Allaah hadhuriki na maasi ya mwenye kuasi wala hanufaishi na utiifu wa mwenye kutii. Utiifu unamnufaisha mwenye nao na maasi yanamdhuru mwenye nao:

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu.”[3]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema katika Hadiyth ya Qudsiy:

“Enyi waja wangu! Lau wa kwanza wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, watakuwa kwenye moyo mmoja wa mtu mwema kabisa miongoni mwenu basi hayo yasingezidisha chochote katika ufalme Wangu. Na lau wa kwanza wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, watakuwa kwenye moyo mmoja wa mtu muovu kabisa miongoni mwenu basi hayo yasingepunguza chochote katika ufalme Wangu.”

Mwishoni mwa Hadiyth hii tukufu anasema (Tabaarak wa Ta´ala):

“Enyi waja wangu! Si vyengine isipokuwa ni matendo yetu ambayo Nakudhibitikieni nayo kisha baadaye Nitakulipeni kwayo. Yule atakayepata kheri basi amshukuru Allaah na yule atakayepata kinyume na hivo asiilaumu isipokuwa nafsi yake mwenyewe.”[4]

Allaah (Ta´ala) anasema:

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ

“Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala sitaki wanilishe.”[5]

Lengo sio kumfanya akatajirika wala akawa na nguvu, kwa sababu amewaumba ili wamwabudu Yeye tu, kitu ambacho manufaa yake yanarudi kwao wenyewe. Aayah hii inabainisha kwamba Tawhiyd maana yake ni ´ibaadah na sio, kama wanavosema wapotevu, kumpwekesha katika uola wa Allaah. Tawhiyd maana yake ni kumtakasia ´ibaadah Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 51:57

[2] 14:08

[3] 39:07

[4] Muslim (6572) na Ahmad (21420).

[5] 51:57

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 08/08/2019