Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa nne: washirikina wa zama zetu ushirikina wao ni wa khatari zaidi kuliko washirikina wa mwanzoni. Washirikina wa mwanzoni walikuwa wakifanya shirki katika kipindi cha raha, wakati katika kipindi cha shida walikuwa ni watakasifu katika ´ibaadah. Ama washirikina wa zama hizi ni wenye kufanya shirki katika kipindi chote, sawa iwe ni wakati wa raha au shida.

MAELEZO

Msingi wa nne – na ndio wa mwisho – ni kuwa washirikina wa leo ushirikina wao ni wa khatari zaidi kuliko washirikina wale ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitumwa kwao. Sababu ya hilo iko wazi. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kuwa washirikina wa kale walikuwa wakimtakasia Allaah ´ibaadah pindi mambo yanapokuwa mazito kwao. Walikuwa hawamuombi mwengine asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall) kwa sababu walitambua kuwa hakuna yeyote anayeokoa kutoka katika matatizo isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Pindi anapokuokoeni katika nchi kavu, mnakengeuka; mtu amekuwa ni mwingi wa kukufuru.” (17:67)

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Na yanapowafunika mawimbi kama vivuli humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”

Bi maana wanamtakasia maombi:

 فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ فَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ

“Lakini anapowaokoa katika nchi kavu, basi miongoni mwao wako mwenye kushika mwendo wa wastani.” (31:32)

Imekuja katika Aayah nyingine:

فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Lakini anapowaokoa katika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha.” (29:65)

Kwa hivyo washirikina wa kale walikuwa wakishirikisha kwa kuyaomba masanamu, miti na mawe katika kipindi cha raha. Ama wanapofikwa na matatizo na wanayaona maangamivu mbele yao, basi wanamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) peke yake na wanayasahau masanamu, miti, mawe na viumbe wengine wote. Ni vipi mtu atamuomba mwengine asiyekuwa Allaah wakati wa raha ikiwa hakuna anayeokoa kutoka katika matatizo isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) peke yake?

Kuhusu washirikina wa zama zetu tukikusudia wale waliokuja nyuma katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliotumbukia katika shirki. Shirki zao zinakuwa nyakati zote sawa katika raha na shida. Hawamwabudu Allaah hata katika kipindi cha matatizo. Bali kila wanapofikwa na matatizo, ndivyo jinsi shirki zao zinavyoongezeka na kumuomba al-Hasan, al-Husayn, ´Abdul-Qaadir, ar-Rafaa´iy na wengineo. Hili ni jambo linalojulikana. Wananasibishiwa vituko mbalimbali vinavyotokea huko baharibini. Pindi mambo yanapowawia mazito huita majina ya mawalii na watu wema na wanawaomba uokozi na msaada badala ya Allaah (´Azza wa Jall). Hili ni kwa sababu walinganizi wa batili na wa upotevu wanawaambia:

“Tutakuokoeni kutokana na bahari. Mkifikwa na kitu basi iteni majina yetu na sisi tutakuokoeni.”

Haya yanapokelewa kutoka kwa wanazuoni wa Suufiyyah. Mnaweza kusoma “Twabaqaat ash-Sha´raaniy”. Humo mna mambo yanayoifanya ngozi kusisimka pindi mtu anaposoma karama za mawalii; wanawaokoa watu kutokamana na mawimbi na wananyoosha mikono yao kwenye bahari na wanabeba boti lote mpaka wanawafikisha nchikavu bila ya mikono yao kulowa. Haya ni baadhi tu ya uongo na ukhurafi wao. Pamoja na kuwa shirki zao ni wakati wote wa raha na shida, ni mbaya zaidi kuliko za washirikina wa kale.

Vilevile Shaykh ametangulia kusema katika “Kashf-ush-Shubuhaat”[1]:

“Watu wa mwanzo walikuwa wakiabudu watu wema katika Mitume, Manabii na mawalii, na ama watu hawa wanawaabudu watenda madhambi ambao wao wenyewe wanalikubali hilo. Wale wanaowaita kuwa ni mabwana na waokozi hawaswali, hawafungi na hawajitengi mbali na uzinzi, liwati na madhambi mengine. Wanaonelea kuwa ´ibaadah haiwawajibikii tena. Ya halali na ya haramu hayatumiki tena kwao, bali ni kwa wasiokuwa wasomi peke yao. Wao wenyewe wanakubali kuwa mabwana wao hawaswali, hawafungi na hawajiepushi na madhambi. Pamoja na hivyo wanawaabudu. Bali wanawaabudu watu ambao ni waovu kabisa. Mfano wa hao ni al-Hallaaj, Ibn ´Arabiy, ar-Rifaa´iy, al-Badawiy na wengineo.”

[1] Tazama “Kashf-ush-Shubuhaat”, uk. 169-170, katika “Mu´allafaat al-Imaam al-Mujaddid”, kitengo cha ´Aqiydah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 18/08/2022