13. Matusi ya al-Waadi´iy juu ya Saudi Arabia ni yenye kutupiliwa mbali

Kuhusu matusi ya Shaykh Muqbil al-Waadi´iy (Rahimahu Allaah) kutukana mamlaka ya Saudia kwa ujumla na khaswakhaswa Mfalme Fahd (Rahimahu Allaah), haya ni maovu tunayoyakemea vibaya sana na tunaona kuwa limeitia dosari Salafiyyah yake. Hata kama ana bidii ya kueneza Sunnah kati ya Raafidhwah na Shiy´ah, alizungumza kwa uwazi katika kitabu “al-Makhraj min al-Fatnah”. Sijakiona na wala sitaki kukiona. Ndani yake ametoa chuki zake juu ya Saudia Arabia, nchi ya Tawhiyd. Inahukumu kwa Shari´ah na inahukumiwa mahakamani. Tawhiyd inafunzwa masomoni na vyuo vikuu. Hakuna makuba yanayotembelewa wala makaburi yanayoabudiwa. Ni nchi ya kipekee ukilinganisha na nchi zengine zote zinazojinasibisha na Uislamu. Hata hivyo hatusemi kuwa haina makosa. Yaliyofanywa na Shaykh Muqbil yamefanywa na wengine pia, akiwemo al-Mas´ariy na Muhammad Suruur, ambao walitumia chuki zao juu ya kuitukana nchi ya Kiislamu na nchi ya upwekeshaji.

Kwa kuzingatia kwamba alikuwa mtu wa Hadiyth anayejinasibisha na mfumo wa Salaf na mwenye kuamini ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, chuki haikutakiwa kumpelekea kiasi hicho, akaiacha Salafiyyah na kwenda katika ushabiki wa muozo na akajitenga mbali na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Pengine akaandika kitabu kingine kinachopingana na hicho kitabu kilichotajwa na akaomba udhuru juu ya makosa yake yaliyotangulia. Allaah atusamehe sisi na yeye na amrudishe katika haki.

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alitaka kumpa mtihani Shaykh Muqbil (Rahimahu Allaah) kwa maradhi. Baadhi ya wanachuoni wema wakajitolea kumpokea ndani ya nchi na kumpa matibabu. Yeye pamoja na familia yake wakafika Saudi Arabia. Nchi ikamkaribisha na kumpokea kwa heshima na wakamkirimu kwa makazi mazuri. Nchi ikagharamia kubaki kwake na gharama za hospitali. Wakati madaktari walipothibitisha kwamba anahitajia matibabu nje ya Saudi Arabia, wakamgharamikia kwenda Marekani kisha baada ya hapo wakamtuma kwenda Ujerumani ili kutibiwa huko. Akatibiwa huko, lakini yeye mwenyewe akachagua arudishwe Saudi Arabia. Akabaki ni mwenye kulala katika hospitali ya kibinafsi ya Mfalme Faysal mpaka alipofariki.

Mimi pamoja na wanachuoni wengine tulienda kumtembelea mara nyingi katika masiku ya Hajj. Nilimpigia simu mara nyingi ili kumjulia hali yake. Kabla ya kufa kwake alirekodi kanda akiisifia nchi hii. Ndani yake alithibitisha kwamba matusi yake yaliyotangulia juu ya mamlaka haruhusu yakachapishwa upya. Alisema wazi tawbah yake juu ya yale yaliyotokea.

Alikufa katika hospitali ya kibinafsi ya Mfalme Faysal huko Jeddah. Aliswaliwa swalah ya jeneza katika msikiti Mtakatifu na akazikwa katika makaburi ya ´Adl. Tunamuomba Allaah amrehemu yeye na sisi na atusamehe sisi na yeye juu ya makosa yetu ambayo hakuna aliyesalimika nayo.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fath ar-Rabbaaniy fiyd-Difaa´ ´an-ish-Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 23/11/2018