al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalizitikisa nyoyo zetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga; tuusie!” Akasema: “Ninakuusieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kusikiliza na kutii hata kama mtataliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu watakasifu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo kwelikweli na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yenye kuzuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni Hasan na Swahiyh.”

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kila ´ibaadah ambayo hawakuabudu kwayo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi na nyinyi msiabudu kwayo. Wale wa mwanzo hawakuwapa wa mwisho la kusema. Mcheni Allaah, enyi wanazuoni, na shikeni njia ya waliokuwa kabla yenu.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud.

ad-Daarimiy amesema: “al-Hakam bin Mubaarak ametukhabarisha: ´Amr bin Yahyaa ametueleza: Nilimsikia baba yangu akieleza kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

“Tulikuwa tukikaa nje ya mlango wa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kabla ya Fajr na anapotoka tunaenda naye mpaka msikitini. Siku moja akatujia Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema: “Abu ´Abdir-Rahmaan ameshakujieni?” Tukasema: “Hapana.” Akakaa na sisi mpaka alipotoka. Alipotoka sote tukasimama. Abu Muusa akamwambia: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hivi karibuni nimeona msikitini kitu nimechokipinga na hakuna nilichoona isipokuwa ni kitu cha kheri tu.” Akasema: “Ni kipi?” Akasema: “Ukiishi utakiona. Msikitini nimewaona watu wamekaa mviringo wakisubiri swalah. Katika kila mviringo kuna mtu na mikononi mwao wana vijiwe vidogovidogo. Anasema: “Semeni: “Allaahu Akbar” mara mia”, wanafanya hivo. Kisha anasema: “Semeni: “Laa ilaaha illa Allaah” mara mia”, wanafanya hivo. Kisha anasema: “Semeni: “Subhaan Allaah” mara mia”, wanafanya hivo.” Akasema: “Uliwaambia nini?” Akasema: “Sikuwaambia kitu. Ninasubiri neno lako au amri yako.” Akasema: “Ungeliwaamrisha wahesabu madhambi yao na kuwadhamini kuwa hakuna chochote katika mema yao kitachopotea.” Halafu akaenda na tukafuatana naye. Alipofika katika mviringo mmoja miongoni mwa miviringo ile akasimama na kusema: “Nini haya ninayoona mnafanya?” Wakasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Ni vijiwe tu ambavyo tunafanya navyo Takbiyr, Tahliyl na Tasbiyh.” Akasema: “Hesabuni madhambi yenu. Mimi ninakudhaminini hakuna chochote katika mema yenu kitachopotea. Ee Ummah wa Muhammad! Ole wenu! Ni haraka iliyoje kuangamia kwenu! Hawa hapa Maswahabah wa Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado wamejaa, nguo zake hazijaharibika na chombo chake hakijapasuka. Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake ima nyinyi mkono katika dini bora kuliko dini ya Muhammad au mmefungua mlango wa upotevu.” Wakasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hatukukusudia jengine isipokuwa kheri tu.” Akasema: “Ni wangapi wenye kuitaka kheri na hawaifikii! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza kuwa kutakuwepo watu wataoisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao. Ninaapa kwa Allaah sijui pengine wengi wao ndio nyinyi wenyewe.” Kisha akatoka pale akenda zake.” ´Amr bin Salamah amesema: “Tuliona wengi katika wao wakishirikiana na Khawaarij siku ya Nahrawaan.”[3]

Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada na Mwenye kutegemewa. Swalah na salamu zimwendee kiongozi wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

[1] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[2] Ibn-ul-Mubaarak katika ”az-Zuhd”, uk. 16, al-Marwaziy katika ”as-Sunnah” (1/30) na Ibn Abiy ´Aasim katika ”as-Sunnah” (1/90).

[3] ad-Daarimiy (204), Bahshal katika ”Taariykh Waaswit” na al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Taariykh Baghdaad” (12/162).

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 42-45
  • Imechapishwa: 23/10/2016