13. Marudilio kwa ufupi ya masomo yaliyotangulia


Tumetangulia kutaja maana ya yale yaliyotajwa na mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) miongoni mwa masuala ambayo ni lazima kwa muislamu wa kiume na wa kike kuyajua.

Ametaja kwamba suala la kwanza ni elimu inayohusu kumtambua Allaah kwa dhati Yake, majina, sifa Zake na kumwamini. Elimu hiyo pia inapelekea kumpenda Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), kumpenda Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale maamrisho na makatazo aliyokuja nayo na mambo ya ´ibaadah ya Kishari´ah juu ya Ummah. Yote hayo ni elimu ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameiteremsha ili itendewe kazi. Waliyofaradhishiwa nayo ni walimwengu wa kibinadamu na kijini.

Kunaingia ndani ya elimu vilevile kumtambua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utambuzi wa Kishari´ah; kumtambua yeye ni nani, amekuja kwa kitu gani na analingania katika kitu gani? Yeye ni Mtume wa Allaah wa kweli aliyetumilizwa na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) rehema kwa walimwengu na akamteremshia kitabu Chake chenye kubainisha ili awalinganie watu na majini kumwabudu Allaah Mmoja na kuacha kuabudu vyengine asiyekuwa Yeye. Kwa hivyo ikawa ni lazima kwa viumbe kumpenda zaidi kuliko wanavyozipenda nafsi zao wenyewe, wazazi, watoto na watu wengine wote[1]. Kwa sababu Allaah amemteua na akamchagua na akamfadhilisha juu ya walimwengu wote. Sababu nyingine Allaah kupitia yeye amewaokoa viumbe katika ulimwengu wa watu na wa majini kuwatoa kwenye viza vya ujinga na janga la upotevu na kuwapeleka katika nuru ya elimu na imani na kumtambua Allaah na yale yanayomuwajibikia Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) katika mambo yanayohusu dini yake.

Kunaingia katika elimu kuijua dini ya Uislamu kwa dalili zake. Dini ya Uislamu ndio dini ambayo Allaah amewausia kwayo Mitume na Manabii wote wawafikishie nayo nyumati zote za ardhini zilizotangulia katika vipindi mbalimbali kuanzia kwa Mtume wa kwanza aliyetumilizwa, ambaye ni Nuuh (´alayhis-Salaam), Allaah amemwamrisha alinganie katika Uislamu. Asili na msingi wake ni kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall) kwa kumpwekesha katika uola Wake, uungu Wake na majina na sifa Zake na matendo Yake yote. Mitume na Mabii wengine wakafuatia – na wale waliolingania kwa kufuata miongozo yao –kwenye kulingania katika dini ya Uislamu, kuutendea kazi na kuacha mengine yasiyokuwa Uislamu mpaka mwishoni ujumbe ukamalizikia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye mlinganizi mkubwa wa Uislamu na mwenye hekima zaidi katika kuulingania. Katika Shari´ah yake kuna uongofu, nuru na rehema. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameufanya Uislamu ndio njia pekee ambayo yule mwenye kuipita hufika katika radhi za Allaah na Pepo Yake katika Nyumba ya karama Yake. Vilevile anasalimika kutokamana na adhabu ya Allaah, hasira na adhabu Yake iumizayo.

Tukirudi katika maana ya Uislamu basi tutajua kwa yakini kabisa kwamba ndio dini ya haki ambayo amelingania kwao kila Mtume aliyetumilizwa na Allaah na kila Nabii aliyetumwa na Allaah. Kila mwanachuoni mlezi alilingania na analingania kwa ulinganizi wa Mitume na Manabii. Uislamu maana yake ni kule kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa utiifu, kujidhalilisha Kwake na kujiepusha na shirki na washirikina. Huu ndio ufunguo wa ujumbe wa kila Mtume na Nabii aliyetumilizwa. Qur-aan tukufu ni dalili na ushahidi bora wa mfumo huu uliofuatwa na Mitume na Manabii wa Allaah na wakapita juu yake wanachuoni walezi katika kila zama na kila mahali katika vipindi mbalimbali vya maisha haya.

Tumejua kupitia suala la pili ambalo ni kuitendea kazi elimu na tumetaja kwamba matendo ndio matunda ya elimu. Kwa sababu elimu yenye manufaa iliyochotwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah ni yenye kuzalisha matendo mema. Elimu na matendo ni mambo mawili yenye kwenda sambamba ambayo moja haliachi jengine. Limoja likiacha jengine kwa njia ya kwamba kukipatikana elimu na kusipatikane matendo ni mwenendo wa wale walioghadhibikiwa. Kukipatikana matendo na kusipatikane elimu ni mwenendo wa wale waliopotea. Kukipatikana elimu na matendo ni mwenendo wa wale walioneemeshwa katika Mitume, wakweli, mashahidi na waja wema. Watu hao wametajwa na Allaah pale aliposema:

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ذَٰلِكَ الْفَضْلُ مِنَ اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ عَلِيمًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao. Hiyo ni fadhilah kutoka kwa Allaah; na inatosheleza Allaah kuwa ni Mjuzi wa yote.”[2]

Miongoni mwa mambo yanayoikamilisha elimu ni kulingania kwayo. Kwa sababu elimu haienei, haifahamiki kwa njia sahihi, Ummah hawanufaiki kwayo isipokuwa wakipatikana wenye kulingania katika elimu hii na wakaitendea kazi. Inatakiwa kulingania katika elimu na matendo. Watu watukufu na watakasifu zaidi ni wale wanaotilia umuhimu jambo la kulingania katika elimu na matendo. Sababu ya utukufu na utakasifu huu ni kwa kuwa wao ndio warithi wa Mitume na warithi wa Mitume. Kwa sababu Mitume na Manabii walikuja kulingania katika elimu na matendo. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akamwongoza kupitia ulinganizi wao yule anayetaka kumwongoza ambao wanastahiki hivo na wakaipa mgongo waliokula maangamivu na wakahukumiwa na Allaah kukoseswa nusura na upotevu kwa sababu hawastahiki jambo hilo – Allaah haulizwi kwa anayoyafanya lakini wao wataulizwa. Haulizwi ni kwa nini amewahukumia watu hao uongofu na akawaongoza na kwa nini amewahukumia watu hao upotevu na akawapoteza. Haya hayasemwi na yule ambaye ana elimu kuhusu dhati ya Allaah na hayasemwi na yule anayemtukuza Allaah ipasavyo. Haya yanasemwa na makafiri, wapotevu na wajinga wasioijua elimu yenye manufaa na matendo mema.

Miongoni mwa nguzo za ulinganizi katika elimu na matendo na miongoni mwa njia zake za Kishari´ah kubwa ni kuwa na subira juu ya maudhi ndani yake, jambo ambalo ni suala la nne:

“Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake.”

Hayo ni kwa sababu mlinganizi ni lazima akabiliane na watu aina mbalimbali wenye ufahamu, mielekeo na viwango vya kutofautiana. Miongoni mwao wako ambao watakubali ulinganizi wake mara ya kwanza tu. Hawa ni wale ambao yamesalimika maumbile yao. Wakilinganiwa kwa Allaah na kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utawaona mara moja ni wenye kukubali, kuipokea na kuipenda.

Utawaona wengine pia baadhi yao wanapuuza ulinganizi wa kheri, wa haki na uongofu kwa sababu ya kujahili kwake kitu ambacho anakihitajia zaidi. Ikiwa mtu huyu anahitajia chakula, kinywaji na kupumua basi anahitajia elimu na matendo kama mfano wa haja yake katika chakula, kinywaji na kupumua. Bali kuhitajia kwake elimu na matendo ndio kukubwa zaidi. Lakini watu wengi hawajui hekima ya kuumbwa kwao.

[1] Shaykh (Rahimahu Allaah) anaashiria Hadiyth iliyopokelewa na Anas ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hatoamini mmoja wenu mpaka niwe ni mwenye kupendwa zaidi kwake kuliko motto wake, baba yake na watu wengine wote.” al-Bukhaariy (01/21) na Muslim (01/67).

[2] 04:69-70

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 29-32
  • Imechapishwa: 24/11/2021