13. Mapendekezo ya kuutembelea msikiti wa Mtume

Swali: Baadhi ya mahujaji wanaona kuwa wasipoweza kuutembelea msikiti wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bais hajj zao zinakuwa na mapungufu. Je, haya ni sahihi?

Jibu: Kutembelea msikiti wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo limependekezwa na sio lazima. Aidha ni jambo halina mahusiano na hajj. Sunnah ni kuutembelea msikiti wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya mwaka mzima. Hilo lisifanywe maalum katika kipindi cha hajj. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kusifungwe safari isipokuwa kuelekea katika misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti huu na msikiti wa al-Aqswaa.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuswali ndani ya msikiti huu ni bora kuliko kuswali ndani ya msikiti mwingine isipokuwa msikiti Mtakatifu.”[2]

Kuna maafikiano juu yake.

Akiutembelea msikiti wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi imesuniwa kwake kuswali Rak´ah mbili Rawdhwah kisha amtolee salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Ni kama ambavo imesuniwa kutembelea al-Baqiy´ na mashahidi kwa ajili ya kuwatolea salamu waliozikwa huko ambao ni Maswahabah na wengineo, kuwaombea du´aa na kuwatakia rehema. Ni kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatembelea. Alikuwa akiwafunza Maswahabah zake wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”[3]

Imekuja katika upokezi mwingine kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa akisema pindi anapotembelea al-Baqiy´:

يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين اللهم اغفر لأهل بقيع الغرقد

Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye. Ee Allaah! Wasamehe watu wa al-Baqiy´ al-Gharqad.”[4]

Vilevile ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa anayetembelea msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuutembelea msikiti wa Qubaa´ na kuswali ndani yake Rak´ah mbili. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiutembelea kila jumamosi na akiswali ndani yake Rak´ah mbili. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayejitwahirisha nyumbani kwake na akaufanya vizuri wudhuu´ wake kisha akauendea msikiti wa Qubaa´ na akaswali ndani yake inakuwa ni kama ´Umrah.”[5]

Haya ndio maeneo yanayotembelewa al-Madiynah al-Munawwarah. Kuhusu msikiti as-Sab´ah, msikiti wa Qiblatayn na maeneo mengineyo yanayotajwa na baadhi ya watunzi wa vitabu kwamba yanatakiwa kutembelewa ni jambo halina msingi na wala halina dalili. Kilichowekwa katika Shari´ah kwa muislamu daima ni kufuata pasi na kuzusha.

[1] al-Bukhaariy (1864) na Muslim (1397).

[2] al-Bukhaariy (1190) na Muslim (1394).

[3] Muslim (974).

[4] Muslim (974).

[5] an-Nasaa´iy (699) na Ibn Maajah (1412).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 56-58
  • Imechapishwa: 03/05/2022