13. Maombi ya kuashiria kwa ajili ya waislamu wenye haja

49- Muslim amepokea kupitia kwa Jaabir ambaye amesema:

“Tulikuwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mchana wakati kundi la watu walio miguu peku na uchi lilipokuja. Nguo zao zilikuwa za kuchanika na panga zao zilikuwa zimenolewa. Wengi wao walikuwa ni kutoka Mudhar. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoona ufakiri walionao sura yake ikabadilika. Akaingia kisha akatoka. Halafu akamuamrisha Bilaal aite kwa ajili ya swalah. Wakaswali na kuhubiri na kusoma:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja na akaumba kutoka humo mke wake na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume wengi na wanawake na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana na jamaa. Hakika Allaah Amekuwa juu yenu Mwenye kuchunga.” (04:01)

na:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mjuzi kwa myatendayo.” (59:18)

Mtu anaweza kutoa swadaqah ya dinari, dirhamu, nguo, ngano hata kipande cha tende.” Mtu mmoja kutoka Answaar akaja na mfuko ambao ulikaribia kumshinda kuubeba. Watu wakaanza kuleta baada yake mpaka nikaona matuta mawili ya chakula na nguo. Uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ukanawiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Atakayeweka katika Uislamu msingi mzuri basi atalipwa ujira kwao na ujira wa yule atakayeufanya pasina kupunguziwa chochote katika ujira wao. Na atakayeweka katika Uislamu msingi mbaya ataadhibiwa kwao na adhabu ya yule atakayeufanya pasina kupunguziwa chochote katika adhabu zao.”[1]

50- Abu Bakr al-Athram amesema:

“Nilisikia jinsi Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal alivyoulizwa juu ya kuomba kwa ajili ya mtu mwingine. Akasema: “Hapana. Afanye hivyo kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.” Wakati waliokuwa miguu peku na uchi walipokuja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Toeni swadaqah.” Hakusema: “Wapeni!” Aliulizwa juu ya mtu mwenye kusema kuwa kuna mwenye kuhitajia ambapo Ahmad akajibu: “Huku ni kwa kuashiria. Ni sawa. Kuomba ni kusema: “Mpeni!” Sionelei mtu kuomba juu ya nafsi yake mwenyewe tusemeje juu ya mtu mwingine. Katika hali hii napendekeza maelezo yasiyokuwa ya moja kwa moja.”

51- al-Firaasiy amesema:

“Je, niombe, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Hapana. Ikiwa hakuna budi basi na awaombe watu wema.”[2]

52- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Shufaieni mtalipwa. Allaah hupanga kupitia kwa Mtume Wake yale anayoyataka.”[3]

Hapa kuna uombaji usiyofungamana [mutlaq] kwa ajili ya mwingine.

53- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si mtu ampe swadaqah huyu?”

54- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake katika hayo. Na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu katika hayo.” (04:85)

Hakusema chochote juu ya kwamba uombezi unakubalika. Ni dalili yenye kuonesha tu kuwa uombezi una thawabu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Shufaieni mtalipwa.”

Haijalishi uombezi umekubaliwa au haukukubaliwa.

57- az-Zuhriy amesema:

“Lau mmoja wenu atakuwa na haja ya ndugu yake basi na aende nyumbani kwake. Ni njia sahali ya kuweza kusaidiwa.”

58- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu´anh) amesema:

“Allaah ana waja ambao watu wanapata utulivu kwao kwa sababu wanasimamia haja zao na wanawafanya wafurahi. Watu hawa ni wenye amani na adhabu ya Allaah siku ya Qiyaamah.”

59- adh-Dhwahhaak amesema juu ya Kauli ya Allaah (Ta´ala):

قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ

“Wakasema: “Ee waziri! Hakika yeye ana baba mkongwe, basi chukua mmoja wetu mahali pake. Hakika sisi tunakuona ni miongoni mwa wafanyao wema.” (12:78)

“Wema wake ilikuwa anapougua mtu jela anamsimamia, wakati mtu anapohisi dhiki anamfanyia wepesi, na pindi mtu anapokuwa na haja anawakusanya watu na kumuombea.”

[1] Muslim (1017).

[2] Abu Daawuud (1646) na an-Nasaa’iy (5/95). al-´Abbaad amesema: ”Dhaifu kwa mujibu wa Shaykh al-Albaaniy.” (Sharh Sunan Abiy Daawuud)

[3] al-Bukhaariy (2/140) na Muslim (16/177).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 45-48
  • Imechapishwa: 18/03/2017