13. Makatazo ya kuzungumza pasi na elimu

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule menye kufikiwa na Hadiyth ambayo haielewi basi atambue kuwa kuna wenye kuielewa na kuimairi kwa ajili yake. Linalompasa ni kuiamini na kuisadikisha. Haijuzu kuwamakinisha akili zao zinazoikadhibisha Hadiyth pamoja na kwamba ni Swahiyh. Haifai kwa muislamu kukadhibisha kitu kama hichi. Lililo juu yake ni kuziamini na asirudishe herufi hata moja kwenye Hadiyth hizo au nyenginezo zilizopokelewa kutoka kwa wapokezi waaminifu.

MAELEZO

Yule ambaye atajahili maana ya Hadiyth juu ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah au Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swiffaat, Qadar au mambo ya halali na ya haramu, basi ni lazima kwake kunyamaza na asizungumze kwa mtazamo wake. Haijuzu kwake akafasiri kwa mtazamo wake. Amesema (Rahimahu Allaah):

“… basi atambue kuwa kuna wenye kuielewa na kuimairi kwa ajili yake.”

Allaah amemtunuku kwa kumpa wanachuoni ambao wamezifasiri Hadiyth ipasavyo. Kwa ajili hiyo utawaona Salaf wakisema kuhusu Hadiyth zinazozungumzai sifa za Allaah:

“Zipitisheni kama zilivyokuja.”

Bi maana kwa udhahiri wake. Wanachuoni wamejua maana zake. Kwa ajili hiyo haijuzu kwa yeyote kuzifasiri kwa kutumia akili yake au kipimo chake. Sifa za Allaah zinathibitishwa kwa Qur-aan na Sunnah. Maoni ya watu hayana nafasi. Maana ya sifa za Allaah iko wazi kabisa. Si kwamba ni mambo yaliyofichikana au yenye kutatiza. Haijuzu kwa yeyote kuyafasiri maandiko pasi na elimu. Haijuzu kumzungumzia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi mna elimu. Kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu ni jambo kubwa kuliko shirki. Amesema (´Azza wa Jall):

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki. Na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[1]

Kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu ni jambo linaingia ndani ya maneno Yake:

وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“… na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”

Kadhalika haijuzu kunasibisha kitu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kimakosa au kukifasiri kinyume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayenisemea uongo kwa kukusudia basi ajiandalie makazi yake Motoni.”[2]

“Kunisemea uongo mimi sio kama kumsemea uongo mwengine. Atakayenisemea uongo kwa kukusudia basi ajiandalie makazi yake Motoni.”[3]

Wanatahadharishwa watu kumsemea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitu ambacho hakikuthibiti, ni mamoja katika kusimulia mapokezi ya Hadiyth au maana zake. Yale maandiko usiyoyajua inakupaswa kunyamaza na uulize. Unatakiwa kukaa kimya na uwaulize wanachuoni ili wakufunze. Ukishajua hapo ndipo unatakiwa kutendea kazi yale uliyojifunza na utalipwa ujira.

[1] 07:33

[2] al-Bukhaariy (110) na Muslim (3).

[3] Muslim (4).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 07/10/2019