Lengo la kumi na tatu: Kujipamba na tabia njema

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kujipamba na tabia njema, adabu kamili, sifa nzuri na adabu kamilifu. Hajj ni masomo bora ya adabu na tabia ambayo muislamu analeleka juu ya tabia nzuri, matangamano mazuri, kujiweka mbali na maudhi, mijadala iliosemwa vibaya na magomvi:

فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ

“Atakayekusudia kuhiji, basi asifanye tendo la ndoa na madhambi wala mabishano katika hajj.”[1]

 “Ambaye atahiji kwa ajili ya Allaah na asizungumze maneno ya kipuuzi wala asifanye tendo la ndoa na wala asifanye madhambi, basi anarejea kama siku ambayo alimzaa mama yake.”

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwaambia watu katika hajj:

“Enyi watu! Utulivu. Utulivu.”[2]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwaambia ile sehemu ya kurusha vijiwe:

“Wasiwaue baadhi yenu wengine.”[3]

 Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj ya kuaga:

“Nisikuelezeni kuhusu muumini? Ni yule ambaye watu wamesalimika na nafsi zao na mali zao. Muislamu ni yule ambaye anawasalimisha waislamu kutokamana na ulimi wake na mikono yake.”[4]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ee ´Umar! Hakika wewe ni mtu mwenye nguvu. Usimuudhi dhaifu. Ukitaka kuligusa jiwe, kusipokuwa watu liguse. Vinginevyo lielekee na useme “Allaahu Akbar.”[5]

Yule mwenye nguvu asizitumie nguvu zake kwa kuwaudhi watu kwa sababu tu eti anataka kulibusu jiwe jeusi hata kama kule kulibusu kwake kutapelekea kuwaudhi wengine. Kwa sababu kitendo cha kulibusu jiwe kimependekezwa ilihali kuwaudhi watu ni jambo limeharamishwa.

Hajj inamlea muislamu juu ya kujipamba na tabia nzuri na pia kujipamba kuwa na subira, urafiki, upole, matangamano mazuri na kuishi vizuri na watu na khaswakhaswa pale atapohisi kuwa mahujaji ni wageni wa Allaah. Hivyo atawafanyia upole, kuwatendea wema na kuwafanyia upole katika kuamiliana nao. Hajj yake ndio itamlea juu ya hayo. Kila pale ambapo mwenye kuhiji atahisi malengo haya makubwa basi atarudi hali ya kuwa ni mwenye kusifika na adabu za Kiislamu na mwenye kujipamba na tabia tukufu za Shari´ah.

Yule mwenye kuhiji anatakiwa katika hajj kuchungana na zile nyakati za kupokelewa du´aa na amuombe Allaah amhidi katika tabia njema, kwani hakuna anayeongoza katika tabia njema isipokuwa Yeye. Vilevile amuombe amuondolee tabia mbaya, kwani hakuna anayeondoa tabia mbaya isipokuwa Yeye.

[1] 02:197

[2] Muslim (1218).

[3] Abu Daawuud katika ”as-Sunan” (1966) na Ahmad katika ”al-Musnad” (16087).

[4] Ahmad (23958).

[5] Ahmad (190).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 66-69
  • Imechapishwa: 22/08/2018