Waliokuwa wamebaki Makkah ilikuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) tu. Walikuwa wamebaki kwa amri yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kulikuwa pia ambao wametiwa mbaroni na washirikina pasi na khiyari yao walikuwa wamebaki.

Abu Bakr alikuwa ameandaa chombo chake na chombo cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku akisubiri Allaah (´Azza wa Jall) ampe rukhusa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kutoka. Usiku mmoja washirikina wakataka kumuua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakateua watu wasimame nje ya mlango wake na kuchunga ili akitoka tu wamuue. Alipotoka nje, hakuna yeyote aliyemwona. Imetajwa katika Hadiyth jinsi alivyoweka udongo kwenye kichwa cha kila mmoja. Kisha akaenda kwenye nyumba ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Wakatoka kupitia pengo la nyumba ya Abu Bakr. Ilikuwa usiku. Alikuwa amemuajiri ´Abdullaah bin Urayqit, alikuwa ni mjuzi wa kuongoza na kuelekeza, kwenda al-Madiynah. Pamoja na kwamba alikuwa katika dini ya mababu zake akamuahidi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usalama. Wakampa kipando chao na wakapanga miadi karibu na pango la Thawr baada ya siku tatu. Walipofika pangoni Allaah akaficha mambo yao na Quraysh hawakuweza kujua ni wapi wameenda.

´Aamir bin Fuhayrah alikuwa akiwaendea na kondoo za Abu Bakr. Asmaa´ bint Abiy Bakr alikuwa akiwapelekea chakula pangoni. ´Abdullaah bin Abiy Bakr alikuwa anasikiliza kinachosemwa Makkah kisha baadaye anawaendea na kuwaeleza kinachoendelea ili wajichunge. Washirikina wakaja kuwatafuta na kufika katika pango la Thawr na maeneo ya jirani yake. Wakapita karibu na maingilio ya pango hilo. Walifika karibu nao kiasi cha kwamba miguu yao ilikuwa kiasi cha urefu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Abu Bakr. Allaah akawaziba macho na hawakuweza kuona maingilio ya pango. Inasemwa – na Allaah ndiye anajua zaidi – ya kwamba buibui ilisuka wavu ambao ulifunika maingilio ya pango na kwamba njiwa mbili zilijenga viota vyao juu yake. Hiyo ndio tafsiri ya Kauli Yake (Ta´ala):

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Msipomnusuru basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: “Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona na Akajaalia neno la waliokufuru kuwa chini. Na Neno la Allaah kuwa ndilo lililo juu. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima, Mwenye hikmah wa yote daima.” (09:40)

Kwa sababu ya hisia zake kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Abu Bakr akaanza kulia wakati washirikina walipopita pembezoni mwao na kusema:

“Ee Mtume wa Allaah! Lau mmoja wao angelitazama kwenye miguu yake basi angelituona.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Abu Bakr! Unafikiriaje juu ya wawili ikiwa Allaah ndio watatu wao?”[1]

Baada ya siku tatu Ibn Urayqit akaja na wale wanyama wawili wa kupanda. Wakapanda juu yake na Abu Bakr akamwacha ´Aamir bin Furayrah akae nyuma yake. Mbele yao mwongozo mwekundu juu ya kipando chake.

Quraysh walikuwa wameahidi ngamia mia moja kwa yule atakayemleta Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Walipopita kabila la Mudlij mkuu wa kabila Suraaqah bin Maalik bin Ju´sham akawaona. Akapande kwenye kipando chake na kuanza kuwatafuta. Alipowakaribia akamsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Qur-aan. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) mara kwa mara anageuka ili kumchunga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anafanya hivo. Abu Bakr akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Huyu hapa Suraaqah bin Maalik ametupata.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaomba du´aa dhidi yake na farasi yake ikaanguka kwa mbele kwenye ardhi. Akasema:

“Nikaanguka. Kilichonipata ni kwa sababu ya du´aa yenu. Niombeeni kwa Allaah ili niweze kuwalinda dhidi ya watu.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuombea na akaachiliwa. Akamuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aandike kitu ambapo Abu Bakr akawa ameandika kwenye kipande cha ngozi. Aliporejea kwa watu wake akawaambia:

“Kilichoko hapa kinawatosheleza.”

Akaja katika Hajj ya kuaga katika sura ya muislamu na akampa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitabu alichomuandikia. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatekeleza alichomuahidi. Mtu huyo alikuwa anastahiki hilo.

Njiani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapita kwenye hema la Umm Ma´bad. Akalala mchana kwake. Akaona alama za utume wake kwenye kondoo na maziwa yake yenye kutoka kwa wingi kabisa kwa muda wa mwaka vinginevyo huwa na ukavu, kitu ambacho kiliwafanya watu wakachanganyikiwa. Swalah na salaam zimwendee!

[1] al-Bukhaariy (4663) na Muslim (2381).

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 32-37
  • Imechapishwa: 18/03/2017