13. Kuamini Qadar hakupingani na kutenda kwa mujibu wa Shari´ah

Kuamini Qadar, kheri na shari yake hakupingani na kutendea kazi Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tendeni! Hakika kila mmoja ni mwenye kufanyiwa wepesi kwa yale aliyoumbiwa.”

Hivyo ndivyo alivyosema pindi alipoulizwa juu ya maana ya matendo ya maisha haya. Je, wino wa kalamu umeshakauka na maamuzi yameshachukuliwa au mambo hayajapangwa? Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kalamu imeshakauka na maamuzi yameshachukuliwa. Walipomuuliza ni ipi sasa faida ya matendo ndio akajibu kwa kusema:

“Tendeni! Hakika kila mmoja ni mwenye kufanyiwa wepesi kwa yale aliyoumbiwa kwayo.”[1]

Wenye furaha wanapata urahisi wa kufanya matendo ya wenye furaha na wenye kula khasara wanapata urahisi wa kufanya matendo ya walaji khasara. Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tendeni!”

kunalengwa kutendea kazi Shari´ah ya Allaah. Kutendea kazi kwa yale waliyokuja nayo Mitume. Watiini Mitume. Allaah amekupa khiyari na uwezo. Amekupa akili ambayo kwa akili hiyo unaweza kupambanua kati ya haki na batili, uongofu na upotevu, utiifu na maasi. Allaah atakufanyia hesabu kutokana na akili hizi Alizokupa. Kwa akili hizi unaweza kupambanua wanyama na vitu visivyokuwa na uhai. Majukumu yako mbele ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) yamefungamanishwa na akili hizo na zenyewe ndio zenye kuamua kama utatakiwa kulipwa au kuadhibiwa.

[1] al-Bukhaariy (4949).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 375-376
  • Imechapishwa: 30/07/2017