2- Jimaa. Swawm inaharibika kwa kufanya jimaa. Mwenye kujamii ilihali amefunga basi swawm yake inaharibika. Katika hali hiyo ni lazima kwake kulipa na kuomba msamaha. Aidha atatakiwa kulipa siku aliyofanya jimaa. Mbali na kulipa atatakiwa kutoa kafara ambayo ni kuacha mtumwa huru, asipopata basi atafunga miezi miwili mfululizo, asipoweza basi atalisha masikini sitini. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimua:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja mtu akisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Una nini? Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ilihali nimefunga.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza. Tulipokuwa katika hali hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na chombo kilicho na tende ambapo akauliza: “Yuko wapi muulizaji?” Akajibu: “Ni mimi hapa.” Akamwambia: “Chukua ukatoe swadaqah.” Akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko watu wa nyumbani kwangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Walishe watu wa nyumbani kwako.”[1]

Kitu kingine kilicho na maana ya jimaa ni kuyatoa manii kwa makusudi. Mfungaji akijitoa manii kwa kutaka kwake mwenyewe kwa kubusu, kupapasapapasa, kujichua sehemu ya siri au mengine basi funga yake inaharibika. Kwa sababu mambo hayo ni katika matamanio ambayo yanaivunja swawm yake. Ni lazima kwake kulipa bila ya kutoa kafara. Kwa sababu kafara hailazimu isipokuwa tu wakati wa kufanya jimaa. Kwa sababu kumepokelewa andiko maalum juu yah ilo.

Ama mfungaji akilala ambapo akatokwa na manii au akatokwa na manii bila ya matamanio – kama mfano wa mwenye maradhi – basi swawm yake haiharibiki. Kwa sababu hakuyafanya hayo kwa kutaka kwake mwenyewe.

[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 157-158
  • Imechapishwa: 23/04/2020