Shaykh Waliyyullaah ad-Dahlawiy amesema:

“Msingi wa hayo ni kwamba kila watu wana siku ambayo wanakusanyika na kutoka katika miji yao wakiwa wamependeza. Hii ni mila ambayo hakuna wasiokuwa nayo, ni mamoja waarabu na wasiokuwa waarabu. Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika Madiynah aliwakuta wanazo siku mbili ambazo wanacheza. Akasema:

“Allaah amewapa badali kwa zilizo bora zaidi; siku ya Adhwhaa na ya Fitwr.”[1]

Imesemekana kuwa siku mbili hizi ilikuwa ni Nayruuz na Mahrajaan. Sababu ya kuzibadilisha ni kuwa hakuna sikukuu yoyote isipokuwa inakuwa na desturi fulani za kidini, imependekezwa na viongozi wa madhehebu au kitu mfano wake. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachelea endapo atawaacha na desturi zao kukahuishwa mambo mbalimbali ya sherehe za kikafiri au desturi za mababu zao. Ndipo zikabadilishwa kwa sherehe za imani ya upwekekaji iliosafi. Pamoja na kupendeza sikukuu mbili hizi zimekusanya pia kumdhukuru Allaah na ´ibaadah ili mkusanyiko wa waislamu usiwe peke yake na furaha pasi na kulinyanyua Neno la Allaah.

´Ibaadah ya kwanza ni siku wanayomaliza swawm na kutoa aina fulani ya zakaah. Hapa kunakusanyika furaha ya kimaumbile, kwa njia ya kwamba wanatua jambo lililowakuia ni gumu kwao na wakati huohuo fakiri anafurahikia zakaah, na furaha ya kubusara, kwa njia ya kufurahikia neema za Allaah alizowaneemesha kwa vile wamefuzu kutekeleza yale Aliyowafaradhishia na kuwaacha wakuu wa familia kubaki mpaka mwaka ujao.

´Ibaadah ya pili ni siku ambayo Ibraahiym alitaka kumchinja mwanae Ismaa´iyl (´alayhimaas-Salaam) ambapo Allaah akamkomboa kwa kumpa kichinjwa kitukufu. Hapa kuna mazingatio na mafunzo ya hali za viongozi wa dini ya upwekekaji ambao walijitolea maisha na mali zao kwa ajili ya kumtii Allaah. Kadhalika kuna makumbusho ya hajj pamoja na kutamani yale waliyomo. Ndio maana imesuniwa kusema “Allaahu Akbar”. Amesema (Ta´ala):

وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Ili mumkabiri Allaah ambaye amekuongozeni.”[2]

Bi maana kushukuru kwa kukuwezesheni kufunga. Ndio maana imesuniwa kuchinja na kusema kwa sauti “Allaahu Akbar” siku za Minaa. Imependekezwa kutonyoa nywele kwa yule aliyenuia kuchinja[3]. Pia ni Sunnah kuswali na kutoa Khutbah ili mikusanyiko yao isikose kuwa na kumdhukuru Allaah na nembo za dini.

Ukiongeza katika haya ni kwamba malengo mengine ya Kishari´ah ambayo ni: kila Ummah unahitaji kuwa na sherehe ambapo watu wanakusanyika ili waonyeshe nguvu na wingi wao. Ndio maana imependekezwa kwa watu wote kutoka ikiwa ni pamoja vilevile na watoto, wanawake, wanawali na wenye hedhi ambao wanatakiwa kujitenga na mahali pa kuswalia na kushuhudia du´aa ya waislamu. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akienda kwa kupita njia moja na mkurudi akipita nyingine ili njia zote mbili ziweze kuona nguvu za waislamu.

Ilipokuwa msingi wa ´Iyd ni mapambo, imependekezwa kuvaa nguo nzuri na kucheza dufu[4], kubadilisha njia na kutoka kwenda mahali pa uwanja.”[5]

[1] Ahmad na wengineo ikiwa na mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Imetajwa katika “as-Swahiyhah” (2021).

[2] 2:185

[3] Anaashiria maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtakapoona mwezi mwandamo wa Dhul-Hijjah na mmoja wenu akataka kuchinja, basi asikate kitu katika nywele zake wala kucha zake.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… asichukue kitu kutoka kwenye nywele zake wala kucha zake mpaka achinje kwanza.” (Mukhtaswar Swahiyh Muslim (1251) na wengineo)

Udhahiri wa Hadiyth unafahamisha kwamba ni wajibu kuacha nywele na kucha kwa yule aliyenuia kuchinja mpaka atakapochinja. Kwa hivyo ni haramu kukata kitu katika hivyo vilivyotajwa. Haya ni maoni ya Imaam Ahmad na wengine. Wale waliopewa mtihani wa kunyoa ndevu wanatakiwa kulitia hili akilini. Kuna dhambi tatu katika kunyoa ndevu:

1- Kile kitendo chenyewe cha kunyoa ni cha kike, kuwaiga makafiri na ni kubadilsha maumbile ya Allaah. Haya nimeyabainisha katika kitabu changu “Aadaab-uz-Ziffaaf”.

2- Kujipamba siku ya ´Iyd kwa kumuasi Allaah.

3- Hadiyth hii inafahamisha kuwa ni haramu kutoa nywele kwa yule anayetaka kuchinja. Uhakika wa mambo ni kwamba ni wachache wenye kusalimika na haya mpaka baadhi ya wanachuoni wametumbukia katika hayo – tunamuomba Allaah usalama!

[4] Anaashiria Hadiyth ambayo imepokelewa na Ibn Maajah (01/391) na wengineo kupitia sanadi mbili. Katika moja kuna Shariyk bin ´Abdillaah al-Qaadhwiy, ambaye hifdhi yake ni dhaifu, na nyingine mna Abu Ishaaq as-Sabi´iy ambaye alikuwa akichanganya mambo. at-Twahaawiy katika “Mushkil-ul-Aathaar (02/209-210) ameitia dosari kwa njia mbili tofauti. Anayetaka anaweza kurejea huko.

[5] Hujjatullaah al-Baalighah (2/30-31).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 38-42
  • Imechapishwa: 13/05/2020