13. I´tikaaf


I´tikaaf ni Sunnah kwa wanaume na wanawake. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf katika Ramadhaan. Njia ya mwisho aliyoitendea kazi ni kwamba alikuwa akikaa I´tikaaf zile siku kumi za Ramadhaan. Ilikuwa ikitokea baadhi ya wakeze wakikaa I´tikaaf pamoja naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakaendelea kufanya hivo baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Lililo bora ni kukaa I´tikaaf katika Ramadhaan. Inaweza kukaliwa katika msikiti wowote ambapo kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliikaa I´tikaaf yale masiku kumi ya Ramadhaan. Kuna wakati aliacha kufanya hivo na badala yake akafanya katika Shawwaal.

Malengo ya I´tikaaf ni kujishughulisha na ´ibaadah na kuwa faragha na Allaah. Kuipa nyongo dunia huku (az-Zuhd) ndiko kulikowekwa katika Shari´ah. Baadhi ya walipokuwa wakifasiri I´tikaaf ya kwamba ni “kukata mawasiliano na wote kwa ajili ya kumtumikia Muumba”. Kwa msemo mwingine ni kukata mawasiliano yote yanayoshughulisha na kumtii na kumuabudu Allaah.

I´tikaaf inafanywa misikitini ambapo kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko. Ikiwa kunaswaliwa swalah ya Ijumaa lililo bora ni kufanya I´tikaaf kwenye msikiti ambapo kunaswaliwa swalah ya Ijumaa ikiwa kuna uwezekano wa kufanya hivo.

Hakuna mudaa maalum uliotengwa kwa ajili ya kufanya I´tikaaf kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni.

Haikushurutishwa mtu kufunga anapofanya I´tikaaf. Lakini hata hivyo lililo bora ni kufunga. Sunnah ni aingie mahala pake pa kukaa I´tikaaf akiwa amenuia I´tikaaf na atoke hapo baada ya kuwa muda wake alonuia umekwisha. Anaweza kukata kukaa kwake kukiwa kuna haja. Kwa kuwa I´tikaaf ni Sunnah. Sio wajibu kuingia katika I´tikaaf maadamu sio ya nadhiri.

Imependekezwa kukaa I´tikaaf zile siku kumi za Ramadhaan. Hivyo ndivyo alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imependekezwa kwa anayeingia katika I´tikaaf aianze tarehe 21 Ramadhaan na atoke pindi yale masiku kumi yameisha. Hivo ndivyo alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kama tulivyotangulia kusema lau ataikata hakuna neno maadamu sio nadhiri. Lau kuna uwezekano mtu atafute sehemu maalum msikitini ambapo mtu anahisi utulivu.

Mwenye kukaa katika I´tikaaf anatakiwa analazimiane na mahala pake pa I´tikaaf na ajishughulishe na kumdhukuru Allaah na ´ibaadah. Asitoke sehemu hiyo isipokuwa wakati wa haja kama kujisaidia na haja ndogo au kubwa. Anaweza vilevile kutoka nje na kwenda kula ikiwa hakupata mtu wa kumletea chakula. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka kwa ajili ya haja zake.

Haijuzu kwa mume kumwingilia mke wake ilihali amekaa katika I´tikaaf. Kadhalika haijuzu kwa mwenye kukaa I´tikaaf kumwingilia mkewe wakati wa I´tikaaf. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[2]

Lililo bora ni kutozungumza sana na watu. Badala yake anachotakiwa ni kujishughulisha na ´ibaadah na kumtii Allaah. Hata hivyo hakuna neno lau atatembelewa na ndugu zake au mwanamke akatembelewa na Mahaarim zake au dada zake na wakazungumza. Wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakimtembelea na wakizungumza. Baada ya hapo wanaenda zao. Hilo linafahamisha kuwa inajuzu.

Inajuzu kwa mwenye kukaa I´tikaaf na wengine kulala na kula msikitini. Kuna Hadiyth na mapokezi juu ya hilo ikiwa ni pamoja vilevile na hali za Ahl-us-Swaffah. Lakini kutilia bidii usafi wa msikiti na kuchunga chakula na vyote vinavyouchafua msikiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeonyeshwa ujira wa Ummah wangu mpaka uchafu ambao mtu anautoa kutoka msikitini.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy na ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuzaymah. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha misikiti ijengwe sehemu za mjini na isafishwe na itiwe manukato[4].

Wameipokea watano isipokuwa an-Nasaa´iy. Mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri.

Ee waislamu! Swawm ni kitendo chema na kikubwa na thawabu zake ni tele na khaswa khaswa swawm ya Ramadhaan. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa kuwa na nia njema na kujitahidi kuhifadhi swawm yake, kusimama nyusiku zake na kukimbilia matendo mema na kutubia madhambi na makosa yote. Tahadharini na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walokataza na mtiini katika Ramadhaan na wakati mwingine. Usianeni na saidianeni juu ya hayo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atukinge sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kutokamana na yale yenye kusababisha ghadhabu Zake na atukubalie sote swawm na visimamo vyetu, awatengeneze watawala wa waislamu na ainusuru dini kupitia wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote kuweza kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] 02:187

[2] 02:187

[3] Abu Daawuud (461) na at-Tirmidhiy (2916). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (2700).

[4] Abu Daawuud (455), at-Tirmidhiy (594), Ibn Maajah (758) na Ahmad (26429). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (436).