Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia Ummah wake Sunnah na kuwawekea nayo wazi Maswahabah zake – nao ndio al-Jamaa´ah. Hili ndio kundi kubwa na kundi kubwa ni haki na watu wake. Mwenye kwenda kinyume na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jambo la dini, amekufuru.

MAELEZO

Kundi kubwa ni wale walio juu ya haki na watu wake walionyooka. Haijalishi kitu hata kama atakuwa ni mtu mmoja peke yake. Kundi kubwa haina maana ya wingi peke yake. Kundi kubwa ni wale walio juu ya haki ijapokuwa watakuwa wachache. Wao ndio kundi kubwa. Hatuangalii wingi bali tunachoangalia ni yale waliyomo. Wengi wanaweza kuwa katika upotevu. Amesema (Ta´ala):

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

“Ukiwatii wengi walioko ardhini, basi watakupoteza kutoka katika njia ya Allaah.”[1]

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Wengi wa watu hawatoamini japokuwa utalikimbilia hilo.”[2]

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِم مِّنْ عَهْدٍ ۖ وَإِن وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ

”Hatukuwakuta wengi wao kuwa ni wakweli wa ahadi. Bali hakika Tumewakuta wengi wao ni mafasiki.”[3]

وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ لَفَاسِقُونَ

”Hakika wengi katika watu ni mafasiki.”[4]

Mtu asidanganyike na wingi isipokuwa ikiwa wako katika haki. Wale walio juu ya haki ndio al-Jamaa´ah. Ni mamoja wakawa wachache au wengi. Kidhibiti ni kuangalia yale waliyomo; ni haki au ni batili. Ikiwa ni haki basi wao ndio al-Jamaa´ah hata kama atakuwa ni mtu mmoja peke yake. Na ikiwa ni batili basi ni upotevu hata kama watakuwa ni watu wengi.

[1] 06:116

[2] 12:103

[3] 07:102

[4] 05:49

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 33
  • Imechapishwa: 23/10/2017