Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

694- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtumzima mzee amepewa ruhusa ya kutofunga. Badala yake atatakiwa kumpa chakula maskini kwa kila siku moja na halazimiki kulipa.”[1]

Ameipokea ad-Daaraqutwniy na al-Haakim. Wote wawili wameisahihisha.

 695- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja mtu akisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Una nini? Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ilihali nimefunga.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza. Tulipokuwa katika hali hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na chombo kilicho na tende ambapo akauliza: “Yuko wapi muulizaji?” Akajibu: “Ni mimi hapa.” Akamwambia: “Chukua ukatoe swadaqah.” Akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko watu wa nyumbani kwangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Walishe watu wa nyumbani kwako.”[2]

Wameipokea wasaba. Tamko ni la Muslim.

MAELEZO

Ni haramu kwa mtu kumjamii mke wake mchana wa Ramadhaan. Ni miongoni mwa vifunguzi vikubwa na kilichokaripiwa zaidi na kinachopelekea katika kafara kubwa. Kafara yenyewe ni kuacha mtumwa huru, asipopata atafunga miezi miwili mfululizo, asipoweza atalisha masikini sitini. Asipoweza hilo pia basi linadondoka.

Bwana huyu ni kama Maswahabah wengine wote alikuwa mwema na alikuwa haoni haya katika jambo la haki. Alikuja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kukiri kuwa amefanya jimaa katika mchana wa Ramadhaan, lakini alikuwa hajui matukio yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamdhihirishia kafara ya kuacha mtumwa huru na akamuuliza kama anaweza kupata mtumwa wa kuacha huru, akamuuliza kama anaweza kufunga miezi miwili mfululizo au kama anaweza kulisha masikini sitini. Kila wakati alipokuwa anaulizwa anajibu hapana. Hatimaye bwana yule akaketi chini pamoja na Maswahabah wengine. Punde kidogo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaletewa tende ambapo akamwamrisha bwana yule azitoe swadaqah kuwapa maskini. Bwana yule akamjibu kwamba Madiynah hakuna masikini zaidi kumshinda ambaye anahitajia tende zile zaidi kumliko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kucheka mpaka magego yake yakaonekana. Zingatia jinsi mtu yule alivokuja akiwa ni mwenye kuogopa kuadhibiwa na akarudi nyumbani na chakula. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Walishe watu wa nyumbani kwako.”

Wala hakumwambia kwamba atoe kafara pale ambapo atapata wasaa wa kufanya hivo. Ni dalili inayojulisha kuwa kafara inadondoka wakati mtu anapokuwa hana uwezo wa kufanya hivo. Pia inalengesha kuwa kufanya jimaa mchana wa Ramadhaan ni dhambi kubwa kwa yule ambaye swawm ni yenye kumuwajibikia.

Wanandoa wote wawili wakiwa ni wasafiri wakati wamefunga. Kisha baadaye wakataka kufanya jimaa. Itafaa? Ndio, itafaa wakaanya jimaa kwa sababu msafiri halazimiki kufunga. Kwa hiyo ikiwa mume na mke wamesfiri kwenda Makkah kufanya ´Umrah na baadaye wakataka kufanya jimaa, wana ruhusa ya kufanya hivo. Aidha hawahitajii kutoa kafara na wala hawapati dhambi. Lakini watalipa siku nyingine badala ya siku hiyo baada ya Ramadhaan.

Huenda wanandoa wawili wamefunga na wako nyumbani na mume akataka kufanya jimaa lakini hata hivyo mke akakataa. Je, inafaa mke akamkatalia? Si kwamba inafaa tu bali ni lazima kwake kumkatalia. Lakini akimlazimisha kufanya jimaa na mke akashindwa kumzuia na hatimaye akamjamii, mume anapata dhambi kwa njia mbili:

1- Ameiharibu swawm yake.

2- Amemlazimisha jimaa mke wake.

Kuhusu mke yeye hapati dhambi. Hahitajii kulipa siku hiyo wala kutoa kafara kwa sababu ni mwenye kupewa udhuru.

[1] ad-Daaraqutwniy (2380) na al-Haakim (1/440).

[2] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/416-422)
  • Imechapishwa: 25/04/2020