13. Hadiyth “Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”


Hadiyth ya nane

8- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Kuna mwanamume alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na juu yake ana funga ya mwezi mzima. Je, nimlipie?” Akamuuliza: “Endapo mama yako angelikuwa na deni ungemfungia?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Kuna mwanamke alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na juu yake ana swawm ya nadhiri. Je, nimfungie?” Akamuuliza: “Unaonaje iwapo mama yako angelikuwa na deni ambapo ukamlipia si ingelihesabika?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi mfungie mama yako.”

Maana ya kijumla:

Katika tukio hili kuna mapokezi mawili. Udhahiri wa mazingira yanaonyesha kwamba ni matukio mawili tofauti na sio tukio moja.

Tukio la kwanza linahusiana na mwanamume aliyekuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamkhabarisha kwamba mama yake amekufa na juu yake ana swawm ya kufunga mwezi mzima na akamuuliza kama anaweza kumlipia.

Tukio la pili linahusiana na mwanamke aliyekuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamkhabarisha kuhusu mama yake ambaye amekufa na juu yake ana swawm ya nadhiri na akamuuliza kama anaweza kumfungia.

Aliwajibu wote wawili kwamba wamfungie mzazi wao. Halafu akawatolea mfano ili maana iwe karibu zaidi na jambo liwe wazi zaidi kwa kuwauliza: “Je, mzazi wenu angelikuwa na deni la mtu si mgemlipia?” Wakajibu: “Ndio.” Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaeleza kwamba swawm hii ni deni la Allaah lililo juu ya mzazi wao. Ikiwa deni la mtu linalipwa, basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Ujumla wa upokezi wa kwanza unatupa faida kwamba maiti anatakiwa kulipiwa swawm yake. Ni mamoja ikawa ni swawm ya nadhiri au kimsingi ni ya wajibu.

2- Upokezi wa pili unafahamisha juu ya kumlipia maiti nadhiri yake.

3- Udhahiri unaonyesha kuwa ni matukio mawili tofauti; tukio la mwanamume na la mwanamke. Kila moja katika hayo yabaki kama yalivyo. Upokezi wa kwanza usifungamanishwe la upokezi wa pili. Kila upokezi ubaki juu ya ujumla wake.

4- Ujumla wa sababu iliyoko katika Hadiyth unahusiana na deni ambalo ni la Allaah, la viumbe, nadhiri ya wajibu au wajibu mwingine kwa msingi wa Shari´ah kwamba yote hayo yanatakiwa maiti alipiwe. Haya yamesimuliwa na mwalimu wetu Shaykh ´Abdur-Rahmaan as-Sa´diy kutoka kwa Taqiyy-ud-Diyn Ibn Taymiyyah (Rahimahumu Allaah).

5- Ndani yake kumethibiti kipimo (Qiyaas), ambayo ni moja katika misingi ya dalili kwa mtazamo wa wanachuoni wengi.  Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatolea mfano kwa jambo ambalo limezoeleka kwao ili waweze kuelewa vizuri.

6- Maneno yake:

“Deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”

ndani yake kuna dalili juu ya kuitanguliza zakaah na haki zengine za Allaah ambazo ni za kimali zikigongana na haki za kimali za watu wengine katika yale aliyoacha maiti. Wako wengine ambao wanaonelea kuwa haki zote hizo ni sawa.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/333-334)
  • Imechapishwa: 08/06/2018