54- Jaabir ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maneno mazuri mno ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo maovu kabisa ni yale yaliyozuliwa. Kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

55- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezua katika amri yetu kisichokuwemo basi atarudishiwa.”[2]

56- ´Abdullaah bin ´Ukaym ameeleza kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akisema:

“Maneno ya kweli kabisa ni maneno ya Allaah. Uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo maovu kabisa ni yale yaliyozuliwa. Kila kilichozuliwa ni Bid´ah.”[3]

57- al-Aswad bin Hilaal ameeleza kwamba ´Abdullaah (bin Mas´uud) (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). “Maneno bora kabisa ni maneno ya Allaah. Hakika mtakuja kuzua na mtakuja kuzuliwa. Kila kitachozuliwa ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

58- ´Abdullaah amesema:

“Fuateni na wala msizue. Kwani mmekwishatoshelezwa. Kila Bid´ah ni upotevu.”[4]

59- Amesema vilevile:

“Hakika sisi tunafuata na wala hatuanzishi kitu wenyewe. Tunafuata na wala hatuzui. Hatutupotea midhali ni wenye kushikamana na mapokezi.”[5]

60- Amesema tena:

“Lazimianeni na elimu kabla haijanyakuliwa. Inanyakuliwa kwa kutoweka wanachuoni. Mtawaona watu wanaodai kwamba eti wanalingania katika Kitabu cha Allaah, ilihali ukweli wa mambo ni kwamba wamekitupa nyuma ya migongo yao. Hivyo lazimianeni na elimu na tahadharini na Bid´ah. Jiwekeni mbali na kujikakama na jiwekeni mbali na kuingia sana kwa ndani na lazimianeni na jambo la lake.”[6]

[1] Muslim (592), Ahmad (3/310) na al-Bayhaqî (3/313).

[2] al-Bukhaariy (2697).

[3] Ibn Naswr (78), Ibn Wadhdhwaah (55), al-Laalakaa-iy (100) na Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Jaami´” (1/158).

[4] Wakiy´ katika ”az-Zuhd” (315), Ahmad (3/110), Ibn Wadhdhwaah (13), Ibn Naswr (81), at-Twabaraaniy (8770) och ad-Daarimiy (211).

[5] al-Laalakaa-iy (105).

[6] al-Bayhaqiy katika ”al-Madkhal” (388).

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 13/12/2018