Tunaamini Qadar kheri na shari yake. Katika kuamini Qadar ndani yake mna daraja nne:

1 – Kuamini kuwa Allaah anayajua yaliyoko sasa na yatayokuweko. Hakuna kitu chenye kujificha Kwake, ni mamoja mbinguni na ardhini. Vilevile hakijifichi Kwake chochote katika yale mambo yenye kujificha yaliyotangulia. Yote inapokuja katika utambuzi wa Allaah (´Azza wa Jall) ni yenye kulingana.

2 – Kuamini kuwa Allaah aliyaandika hayo katika Ubao uliohifadhiwa. Humo kumeandikwa makadirio ya kila kitu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu cha kwanza ambacho Allaah alianza kuumba ni kalamu halafu akaiambia: “Andika!” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatayokuwepo hadi siku ya Qiyaamah.””[1]

Tunaamini kuwa kila kinachopitikika na kutokea Allaah amekijua na Allaah akakiandika katika Ubao uliohifadhiwa. Amesema (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[2]

Hakuna kadirio lolote ndani ya Ubao uliohifadhiwa ambalo linabadilishwa. Makadirio yaliyoandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa ni jambo limetangulia miaka 50.000 kabla ya kuumba mbingu na ardhi. Imethibiti katika Hadiyth ambayo ni Swahiyh ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa hakuna kitu isipokuwa kimeandikwa katika Ubao uliohifadhiwa. Amesema (Ta´ala):

وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ

“Tunacho Kitabu kinachohifadhi.”[3]

3 – Kuamini matakwa ya Allaah yaliyoenea na utashi Wake juu ya kila kitu. Vilevile tunaamini kuwa Allaah akilitaka jambo – matakwa Yake ya kilimwengu – basi ni lazima litokee. Hakuna kitu kinachotokea katika ulimwengu isipokuwa kwa matakwa na makadirio ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

4 – Kuamini – na hii ndio ngazi ya mwisho – ya kwamba kila kitu kimeumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

“Allaah ndiye Muumbaji wa kila kitu Naye juu ya kila kitu ni mdhamini anayetegemewa.”[4]

Kila kilichomo katika ulimwengu, kuanzia kilichokuwepo na kitachokuwepo, kimeumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote katika ulimwengu anayeumba kitu asiyekuwa Allaah.

[1] at-Tirmidhiy (2155) na Abu Daawuud (4700).

[2] 57:22

[3] 50:04

[4] 39:62

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 24/05/2022