13. Baadhi ya fadhilah za elimu na wanachuoni

Elimu inazo fadhilah nyingi ikiwa ni pamoja na zifuatazo:

1 – Allaah huwanyanyua wanachuoni Aakhirah na duniani. Kuhusu Aakhirah Allaah atazinyanyua daraja zao kutegemea na vile walivyolingania katika dini ya Allaah na kutendea kazi yale waliyoyajua. Duniani Allaah atawanyanyua kati ya waja Wake kutegemea na yale waliyofanya. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu zaidi.”[1]

2 – Ni mirathi ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Mitume hawarithiwi dinari wala dirhamu. Lakini si vyenginevyo wanachorithiwa ni elimu. Hivyo basi yule mwenye kuinyakua basi amejinyakulia fungu kubwa.”[2]

3 – Ni miongoni mwa yale mambo ya mtu yanayobaki baada ya kufa kwake. Imethibiti katika Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu hukatika matendo yake yote isipokuwa vitu vitatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu hunufaika kwayo au mtoto mwema mwenye kumwombea.”[3]

4 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupendeza mtu kumfanyia hasadi ilionzuri mwingine juu ya neema yoyote isipokuwa katika neema mbili:

  • Kuitafuta elimu na kuitendea kazi.
  • Tajiri ambaye ameifanya mali yake kutumikia Uislamu.

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna hasadi isipokuwa katika mambo mawili; mtu ambaye amepewa mali na Allaah akaiangamiza katika haki na mtu mwingine ni yule ambaye Allaah amempa elimu na akawa anahukumu kwayo na anaielimisha.”[4]

5 – Elimu ni nuru ambayo mja anaangaza kwayo ambapo anajua namna gani atamwabudu Mola wake na namna atakavotangamana na wengine. Hivyo mapito yake yanakuwa juu ya elimu na utambuzi.

6 – Elimu ni nuru ambayo mwanachuoni anapata kuwaongoza watu kwayo katika mambo ya dini na dunia yao. Wengi wenu mnatambua kiasi cha yule bwana wa wana wa israaiyl ambaye aliua nafsi 99 akamuuliza mwema mmoja kama anaweza kutubia. Kana kwamba mwema huyo alikuza jambo lake na kumwambia kwamba hawezi kutubia. Matokeo yake muulizaji yule akamuua na ikatimia idadi ya 100. Halafu akaenda kwa mwanachuoni akamuuliza ambapo akamweleza kwamba anaweza kutubia na kwamba hakuna chochote kiwezacho kumzuia yeye na kutubia. Lakini akamwelekeza katika nchi ambayo wakazi wake ni wema atoke aende huko. Akatoka kuelekea huko na kifo kikamkuta njiani. Kisa kinatambulika. Tazama tofauti kati ya mwanachuoni na mjinga!

[1] 58:11

[2] at-Tirmidhiy (2691), Abu Daawuud (3641) na Ibn Maajah (223). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Ibn Maajah” (182).

[3] Muslim (1631).

[4] al-Bukhaariy (73) na Muslim (716).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 22/06/2021