13. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati na kati


3- Kundi la tatu: Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wao wako kati na kati baina ya madhehebu mawili; madhehebu ya Murji-ah na madhehebu ya Khawaarij. Wao wanaoanisha baina ya maandiko na wanasema: Kufuru na shirki ndani ya Qur-aan na Sunnah vimegawanyika mafungu mawili; kufuru kubwa na kufuru ndogo,  shirki kubwa na shirki ndogo. Vilevile kuna madhambi yaliyo chini ya kufuru hayamfanyi mtu kuwa kafiri.

Kuhusu shirki na kufuru kubwa vinamtoa mtu katika Uislamu. Lakini kufuru na shirki ndogo havimtoi mtu katika Uislamu. Tofauti na wanavyoonelea Khawaarij. Lakini hata hivyo vinaipunguzaiImani. Tofauti na wanavyoonelea Murji-ah. Makundi hayo mawili yanagongana. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah  – na himdi zote anastahiki Allaah – wako kati na kati na wanaoanisha kati ya maandiko yanayozungumzia ahadi na maandiko yanayozungumzia matishio. Vilevile wamekusanya kati ya khofu na matarajio. Hawakuchukua matarajio peke yake, kama walivofanya Murji-ah, na hawakuchukua khofu peke yake, kama walivofanya Khawaarij.

Mwenye kumuabudu Allaah kwa khofu peke yake ni Khaarijiy. Mwenye kumuabudu Allaah kwa matarajio peke yake ni Murjiy. Mwenye kumuabudu Allaah kwa mapenzi peke yake ni Suufiy. Lakini yule mwenye kuamuabudu Allaah kwa khofu, matarajio, mapenzi na kutaraji, shauku na kuogopa ndiye mpwekeshaji Sunniy.  Huu ndio ufafanuzi kuhusu masuala haya makubwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 08/05/2018