129. Kufaradhishwa kwa nguzo ya kwanza, ya pili na ya tatu


Maneno yake (Rahimahu Allaah):

Akafaradhishiwa juu yake swalah tano kwa siku. Aliswali Makkah kwa miaka mitatu.

Alikuwa akiziswali Rak´ah mbilimbili. Wakati alipohajiri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio akawa anakamilisha zile swalah za Rak´ah nne isipokuwa tu Fajr ambayo inatakiwa kurefushwa ndani yake kisomo na ikabaki Rak´ah mbili kama ilivyo. Vinginevyo Maghrib ilikuwa ni Rak´ah tatu tokea mwanzo ilipofaradhishwa kwa sababu ni Witr ya mchana. Kuhusu Dhuhr, ´Aswr na ´Ishaa Makkah ilikuwa Rak´ah mbilimbili. Pindi alipohajiri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akazikamilisha Rak´ah nne. Imepokelewa katika Hadiyth:

“Mwanzoni ilipofaradhishwa swalah ilikuwa Rak´ah mbilimbili. Wakati alipohajiri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakamilisha swalah hali ya ukazi na kukabaki swalah katika hali ya safari.”[1]

Haya ni kwa maafikiano ya wanachuoni kwamba swalah ilifaradhishwa Makkah na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alianza kuiswali Makkah. Lakini wametofautiana kama ilifaradhishwa miaka mitatu kabla ya kuhajiri? Haya ndio maoni yenye nguvu kama alivyotaja Shaykh hapa. Kuna maoni yanayosema ni miaka mitano, mwaka mmoja na maoni mengine mwaka mmoja na nusu kabla ya kuhajiri. Lakini hata hivyo maoni yenye nguvu zaidi ni kama alivosema Shaykh kwamba ni miaka mitatu kabla ya kuhajiri.

Je, kuna kitu kingine kilichofaradhishwa pamoja na swalah? Hapa ni mahali ambapo wanachuoni wametofautiana. Miongoni mwao wako wenye kuona kwamba zakaah pia ilifaradhishwa Makkah. Lakini kiwango cha zakaah, kiasi chake na wenye kuistahiki ndivo vilivyobainishwa Madiynah. Ama msingi wa kufaradhishwa kwake ilikuwa Makkah. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

“Toeni haki yake [zakaah] siku ya kuvunwa kwake.”[2]

Makusudio ya haki hapa ni zakaah. Jengine ni kwamba Suurah yote imeteremshwa Makkah. Vilevile katika maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ

”Na wale ambao katika mali zao kuna haki maalum, kwa ajili ya mwombaji na asiyeomba kwa kujistahi.”[3]

pia ni Suurah iliyoteremshwa Makkah. Makusudio ya “haki maalum” ni zakaah. Msingi wake umefaradhishwa Makkah. Lakini upambanuzi wake umebainishwa Madiynah. Haya ni maoni ya kwanza.

Maoni ya pili – na ndio yanayodhihiri kutoka katika maneno ya Shaykh hapa – ni kwamba zakaah ilifaradhishwa Madiynah. Hakuna kilichofaradhishwa Makkah isipokuwa nguzo ya kwanza ambayo ni Tawhiyd na nguzo ya pili ambayo ni swalah. Huu ndio udhahiri wa maneno ya Shaykh.

[1] al-Bukhaariy (350) na Muslim (685).

[2] 06:141

[3] 70:24-25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 259-261
  • Imechapishwa: 09/02/2021