128. Alisafirishwa (صلى الله عليه وسلم) kwa roho na kiwiliwili


Ni lazima kuamini kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisafirishwa usiku na akapandishwa juu mbinguni kwa roho na kiwiliwili chake vyote hali ya kuwa macho na si usingizini. Kwa sababu baadhi ya watu wanasema kuwa alisafirishwa usiku kwa roho yake na kwamba kiwiliwili chake kilibaki Makkah na kwamba alisafirishwa usiku na akapandishwa juu kwa roho yake. Maneno haya ni batili. Bali alisafirishwa usiku kwa roho na kiwiliwili chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa juu ya mnyama. Hayo yalipitika akiwa macho na si usingizini. Kwa maana ingelikuwa ni kwa roho yake pekee au ingelikuwa ni usingizini, ni vipi tofauti kati yake na ndoto?

Isitoshe Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِه

”Utakasifu ni wa ambaye alimsafirisha usiku mja Wake.”[1]

Neno mja hutumika juu ya roho na mwili vyote viwili. Neno hilo halitumiwi juu ya roho peke yake kwamba ni mja kama ambavo kiwiliwili peke yake hakitwi kuwa ni mja. Mja hutumiwa juu ya roho na mwili vyote kwa pamoja. Hakusema:

سبحان الذي أسرى بروح عبده

”Utakasifu ni wa ambaye alisafirisha usiku roho ya mja Wake.”

Bali alisema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِه

”Utakasifu ni wa ambaye alimsafirisha usiku mja Wake.”

Mja hutumiwa juu ya roho na mwili vyote kwa pamoja. Allaah (Jalla wa ´Alaa) hashindwi na chochote. Yeye juu ya kila jambo ni muweza.

[1] 17:01

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 259
  • Imechapishwa: 09/02/2021