127. Safari ya Mtume (صلى الله عليه وسلم) kupandishwa mbinguni na kufaradhishiwa swalah tano

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya miaka kumi alipandishwa mbinguni na akafaradhishiwa juu yake swalah tano kwa siku. Aliswali Makkah kwa miaka mitatu.

MAELEZO.

Baada ya miaka kumi… – Alibaki (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) miaka kumi akiwa juu ya hali hii akikataza shirki na akilingania katika Tawhiyd na akisimika msingi huu. Halafu katika mwaka wa kumi na moja akasafirishwa kutoka msikiti Mtukufu na kwenda msikiti wa al-Aqswaa. Amesema (Ta´ala):

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote daima, Mwenye kuona yote daima.”[1]

Wakati ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amelala kwenye nyumba ya Umm Haaniy´ alimjia Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja naye mnyama kwa jina “Buraaq”, mdogo kuliko nyumbu na mkubwa kuliko punda. Hatua yake inapiga kwenye upeo yanapofika macho yake. Akampanda (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasafiri naye kwenda Yerusalemu wakati wa usiku.

Hii ni sifa maalum kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni miongoni mwa miujiza yake. Huko Yerusalemu alikutana na Mitume wengine. Kisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapandishwa juu mbinguni kutokea Yerusalemu kwenda juu mbinguni akiandamana na Jibriyl. Jibriyl alimpandisha na akawapita wakazi wa mbinguni. Kila mbingu Jibriyl akibisha hodi na anafunguliwa. Akafika mpaka mbingu ya saba. Kisha akapanda juu ya mbingu ya saba mpaka kwenye mkunazi. Hapo ndipo Allaah (´Azza wa Jall) alimzungumzisha kwa Wahy Wake kwa aliyoyataka na akamfaradhishia swalah tano. Alimfaradhishia swalah khamsini mchana na usiku lakini hata hivyo Muusa akamwashiria Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) amwombe Mola Wake amfanyie wepesi na kwamba Ummah wake hautoweza swalah khamsini mchana na usiku. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) akawa ni mwenye kuendelea kumwomba Mola Wake wepesi mpaka zikaishilia katika swalah tano. Allaah (´Azza wa Jall) akasema kama ilivyopokelewa katika Hadiyth ya Israa´ na Mi´raaj:

“Faradhi Yangu imekwishapita, nimewakhafifishia waja Wangu na nitalipa jema moja kwa kumi.”[2]

Katika upokezi mwingine uliopekelewa na Anas kupitia kwa Abu Dharr alisema:

“Ni tano lakini ni khamsini.”[3]

Bi maana ni tano kimatendo na ni khamsini katika mizani.

Swalah tano mchana na usiku zinazingatiwa kuwa swalah khamsini kwenye mizani. Kwa sababu jema moja linalipwa kwa kumi na mfano wake. Swalah moja inalipwa kwa swalah kumi.

Kusafirishwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumetajwa mwanzoni mwa Suurah  “Subhaanah” ambayo ni Suurah “Banuu israaiyl”.

Kupandishwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu mbinguni kumetajwa mwanzoni wa Suurah “an-Najm”:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ

“Kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine, kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa, karibu yake kuna bustani ya al-Ma´waa, pindi ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika, jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka. Hakika aliona miongoni mwa alama za Mola wake kubwa kabisa.”[4]

Huku ndio kupandishwa juu mbinguni.

Kisha akateremka kutoka mbinguni na kwenda Yerusalemu. Halafu akarjea Makkah katika usiku wake. Wakati kulipopamazuka na akawaeleza watu jambo hilo waumini imani yao iliongezeka na makafiri shari yao ikaongezeka na walifurahishwa kwa jambo hilo na wakawa wakilitangaza na kuwauliza watu ni vipi rafiki yao anaweza kudai kuwa amekwenda Yerusalemu na akarudi kwenye usiku mmoja ilihali wao wanaenda kwa mwendo wa ngamia mwezi mmoja kwenda na mwezi mmoja kurudi. Wanalinganisha uwezo wa Muumba na uwezo wa viumbe! Kwa hiyo jambo hili ilikuwa ni Allaah (´Azza wa Jall) anataka kuwatahini watu. Washirikina uovu, shari na kumtukana kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kukaongezeka na waumini imani yao ikazidi. Kwa ajili hii wakati washirikina walipomwambia Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mtazame rafiki yako ni nini anachosema?” Akasema: “Kwani amesema nini?” Wakasema: “Anadai kuwa ameenda Yerusalemu na akapandishwa juu mbiguni na kwamba akaja ndani ya usiku mmoja.” Abu Bakr as-Swiddiyq akasema: “Ikiwa amesema hivo basi mambo ni kama alivosema. Amesema kweli.” Wakasema: “Vipi inakuwa hivo?” Akasema: “Mimi namsadikisha kwa yaliyo makubwa zaidi kuliko hayo. Mimi namsadikisha juu ya khabari za mbinguni zinazomteremkia. Ni vipi nisimsadikishe juu ya kusafirishwa usiku kwenda Yerusalemu?”[5]

Haya ni kwa uwezo wa Allaah na si kwa uwezo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ni kwa uwezo wa Allaah na ni katika miujiza ya Mtume Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni katika karama zake kutoka kwa Mola Wake (´Azza wa Jall).

[1] 17:01

[2] al-Bukhaariy (3207) (3887).

[3] al-Bukhaariy (349).

[4] 53:13-18

[5] al-Haakim (03/65) (3307).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 255-259
  • Imechapishwa: 09/02/2021