Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Miaka kumi alilingania katika Tawhiyd.

MAELEZO

Miaka kumi… – Bi maana Makkah. Alikuwa ni mwenye kukataza shirki. Kwa sababu walikuwa ni wenye kuyaabudu masanamu. Hekima ya Allaah kumtuma Makkah ni kwa sababu Makkah ndio mji mkuu ambao miji yote inarejea huko. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ حَتَّىٰ يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًاَ

“Mola wako hakuwa Mwenye kuiangamiza miji mpaka apeleke katika miji mikuu yake Mtume.”[1]

Mji mkuu ni marejeo ambao unarejelewa na msingi unaorejelewa. Huo ndio mji mkuu. Amesema (Ta´ala):

هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ

Nazo ndio msingi wa Kitabu.”[2]

Msingi ambao kunarudishwa Aayah zinazotatiza. Vivyo hivyo Makkah, iliyoheshimishwa na Allaah, ndio msingi ambao wanarejea kwake watu wa ulimwenguni na waislamu kutoka katika kila pembe ya dunia wanarejea Makkah. Ndio mji mkuu ikiwa na maana ya marejeo. Kwa ajili hiyo Allaah akamtumiliza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokea Makkah kwa sababu ndio mji mkuu. Aliishi ndani yake kwa miaka kumi na tatu akikataza wakazi wa Makkah shirki na akiwaamrsha Tawhiyd. Kwa sababu watu wa Makkah ndio kiigizo chema kwa wengine.  Kwa ajili hiyo Makkah inatakiwa kubaki, mpaka siku ya Qiyaamah, kuwa ni mji wa Tawhiyd na taa la kulingania kwa Allaah. Sambamba na hayo yatengwe mbali yale yote yanayokwenda kinyume na hayo kama mfano wa shirki, Bid´ah na mambo ya ukhurafi. Kwa sababu watu siku zote na kila mahali wanaitazama Makkah. Yanayofanywa ndani yake yanaenea ulimwenguni. Ikiwa yanayofanywa ndani yake ni kheri basi kheri inaenea na ikiwa yanayofanywa ndani yake ni shari basi shari inaenea. Ndio maana Makkah inatakiwa kusafishwa daima. Kwa ajili hii amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ

“Tulichukua ahadi kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl kwamba waisafishe Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaofanya i’tikaaf na wanaorukuu na kusujudu.[3]

Ni lazima kuisafisha Makkah kutokamana na kila kitu kinachokwenda kinyume na Uislamu ili kutoke ndani yake dini na ulinganizi mashariki na magharibi mwa dunia. Kwa sababu Allaah amemtuma Mtume Wake kutoka humo na akaanza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulinganizi wake humo.

Aliishi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Makkah miaka kumi na tatu. Katika hiyo kuna kumi akiwalingania watu katika Tawhiyd na akiwakataza shirki. Hakuamrisha kitu kingine zaidi ya hicho. Hakuamrisha swalah, zakaah, swawm wala hajj. Bali Da´wah yake ilikuwa imefupika juu ya kuonya kutokamana na shirki na kuamrisha Tawhiyd. Alikuwa akiwaambia “Semeni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah´ mtafaulu na wao wakisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[4]

[1] 28:59

[2] 03:07

[3] 02:125

[4] 38:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 253-255
  • Imechapishwa: 08/02/2021