Ibn ´Abdil-Wahhaab amesema:

“Allaah Amemtuma ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd.”

Huu ndio ulinganizi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ilikuwa kuonya shirki na kulingania Tawhiyd. Huu ndio mfumo ambao walinganizi wanatakiwa kupita juu yake. Wanatakiwa kabla ya kila kitu kutilia mkazo kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd. Vinginevyo Da´wah yao itakuwa si yenye kufuata mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah amemtuma Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd. Kwa hiyo ni lazima kwanza kuweka msingi wa kitu hichi. Baada ya hapo ndio mtu aende katika mambo mengine. Kwa sababu hayatengemai mambo pasipokuweko Tawhiyd. Endapo watu wataacha uzinzi, pombe, wizi na wakasifika kwa kila sifa nzuri katika matendo na tabia lakini wasiache shirki, basi hakuna faida ya mambo haya na hayatowanufaisha kitu. Upande wa pili ni kwamba mtu akisalimika kutokamana na shirki na wakati huohuo akawa na madhambi makubwa ambayo ni chini ya shirki basi mtu huyo bado kuna matarajio ya Allaah kumsamehe au akamuadhibu kwa kiasi cha mdhambi yake. Lakini hata hivyo mafikio yake ya mwisho ni Pepo kwa sababu ni mpwekeshaji.

Kwa hiyo Tawhiyd ndio msingi. Hakuna kusalimika pasipokuwa na Tawhiyd. Kwa ajili hiyo ndio maana inatakiwa kutilia mkazo, kuitilia manani siku zote na kila mahali, kuwalingania watu kwayo na kuwafunza nayo. Pia inatakiwa kuwabainishia watu Tawhiyd; maana ya Tawhiyd na maana ya shirki. Ni lazima kwa muislamu ayajue mambo haya, ayaepuke kabisa na aichunge nafsi yake ili asije kutumbukia katika kitu katika shirki au akaiharibu Tawhiyd. Ni lazima kupatikane jambo hili. Ni lazima kwa Da´wah isimame juu ya msingi huu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 253
  • Imechapishwa: 08/02/2021