124. Namna Mtume (صلى الله عليه وسلم) alivyopewa utume


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Alipewa utume kwa “al-Muddaththir”. Mji wake ni Makkah.

Allaah Amemtuma ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze! Na nguo zako zitwaharishe! Maambukizi yote ya kishirikina epukana nayo! Na wala usitoe kwa kwa kutaraji kukithirishiwa! Na kwa ajili ya Mola wako subiri!”[1]

قُمْ فَأَنذِرْ

“Simama na uonye!”

maana yake ni kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd.

وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ

“Na Mola wako mtukuze!”

Maana yake amtukuze kwa Tawhiyd.

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Na nguo zako zitwaharishe!”

Maana yake twahirisha matendo yako kutokana na shirki.

وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ

“Maambukizi yote ya kishirikina epukana nayo!”

Ni masanamu. Kuyakata, ina maana ya kuyaepuka na kujitenga nayo na watu wake.

MAELEZO

Kisha akateremkiwa na maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye!”

Huku ndio kutumilizwa na hii ndio maana ya maneno ya Shaykh:

“Alipewa unabii kwa “Iqra´” na akapewa utume kwa “al-Mudaththir”.

Tofauti kati ya Nabii na Mtume ni kwamba Nabii ni yule mwenye kuteremshiwa Shari´ah na asiamrishwe kuifikisha. Mtume ni yule mwenye kuteremshiwa Shari´ah na akaamrishwa kuifikisha. Kuweka wazi zaidi jambo hilo ni kwamba Mtume anateremkiwa na Shari´ah na Kitabu.

Alikuwa nabii kwa Iqra´ na akatumilizwa kwa al-Mudaththir mwanzoni mwanzoni mwa miaka arubaini. Vivyo hivyo Manabii wengine. Jengine ni kwamba Nabi anatumilizwa kwa Shari´ah ya waliyekuwa kabla yake, Kitabu cha aliye kabla yake na anatimiziwa baadhi ya mambo kama Manabii wa wana wa israaiyl baada ya Muusa.

al-Mudaththir maana yake ni kujigubika. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipatwa na kitu katika woga ambapo akasema: “Nigubikeni, nigubikeni.” akimaanisha afunikwe. Ndipo Allaah akamteremshia:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze!”

Bi maana mtukuze.

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

”Na nguo zako zitwaharishe!”

Bi maana yatakase matendo yako kutokamana na shirki. Matendo pia huitwa vazi. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ

“Enyi wana wa Aadam! Hakika Tumekuteremshieni mavazi yanayoficha sehemu zenu za siri na nguo za pambo; na vazi la kumcha Allaah ndiyo bora zaidi.”[2]

Ameita taqwa kwamba ni vazi.

Maambukizi  – Bi maana masanamu.

Epukana nayo – Bi maana yaache na jitenge nayo mbali.

Allaah akamtumiliza alipokuwa na arubaini.

Alibaki Makkah miaka kumi na tatu akiwalingania watu katika Tawhiyd na kuacha kuyaabudu masanamu. Kulitokea mabadiliko ya hali kati yake yeye na washirikina. Kulitokea juu yake maudhi na kwa wale waliomwamini na kumfuata. Walipatwa na kero kutoka kwa washirikina ndani ya miaka hii kumi na tatu.

Miaka mitatu kabla ya kuhajiri alisafirishwa kwenda Yerusalemu na akapandishwa mbinguni. Alifaradhishiwa vipindi vya swalah tano na akaswali Makkah kwa miaka mitatu. Kisha Quraysh wakafanya njama za kumuua. Ndipo Allaah akampa idhini ya kuhama kwenda Madiynah ambapo akahajiri kwenda Madiynah baada ya kukutana na Answaar katika bay´ah ya ´Aqabah ya kwanza na bay´ah ya ´Aqabah ya pili.

Alihama kwenda Madiynah na akaishi ndani yake miaka kumi na kwa jumla miaka ishirini na tatu. Baada ya kupewa unabii aliishi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) miaka kumi na tatu. Miaka kumi na tatu hii alikuwa akiweka msingi wa Tawhiyd Makkah na miaka kumi Madiynah.

Kisha Allaah akamfisha mwanzoni mwanzoni mwa miaka sitini na tatu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Muda wa umri wa ujumbe wake ni miaka ishirini na tatu. Baraka yote hii ambayo Allaah (´Azza wa Jall) aliyoiteremsha juu yake, elimu hii tukufu, jihaad hii na tamkini hii katika muda huu mfupi ni ndani ya miaka ishirini na tatu. Haya ni miongoni mwa miujiza ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni miongoni mwa baraka za Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), baraka za ulinganizi wake na baraka za Wahy aliyoteremshiwa. Kabla ya yote hayo ni msaada wa Allaah (´Azza wa Jall). Yeye ndiye kamsaidia, Yeye ndiye kamhami na akamnusuru mpaka ulinganizi wake ukafika mashariki na magharibi. Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] 74:01-07

[2] 07:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 249-253
  • Imechapishwa: 08/02/2021