123. Namna Mtume (صلى الله عليه وسلم) alivyopewa unabii


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aliishi kwa umri wa miaka sitini na tatu, arubaini kabla ya utume na ishirini na tatu kama Nabii na Mtume. Alipewa unabii kwa [kupewa Suurah] “Iqra´”

MAELEZO

Alizaliwa Makkah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akanyonyeshwa kwa Banuu Sa´d kwa Haliymah as-Sa´diyyah. Baba yake ´Abdullaah alikufa akiwa ndani ya tumbo la mama yake. Baadaye kidogo baada ya mama yake kumzaa naye akafariki. Umm Ayman al-Habashiyyah, ambaye alimrithi kutoka kwa baba yake, akamwangalia. Akawa chini ya uangalizi wa babu yake ´Abdul-Muttwalib. ´Abdul-Muttwalib akafariki na uangalizi ukahamia kwa ami yake Abu Twaalib.

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliishi miaka arubaini kabla ya kupewa unabii akiwa ni mwenye kutambulika kwa uaminifu, ukweli na ukarimu. Katika kipindi hicho alikuwa ni mwenye kujiepusha na kuabudu masanamu na kunywa pombe. Hakuwa ni mwenye kufanya mambo yanayofanywa na watu wa kipindi cha kikafiri. Bali yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka kwenda katika pango la Hiraa´ na akifanya ´ibaadah kwa masiku kadhaa na akimwabudu Allaah kutokana na mila ya Ibraahiym juu ya Tawhiyd.

Alipofikisha umri wa miaka arubaini (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akateremkiwa na Wahy kwa njia ya kwamba alimjia Jibriyl akiwa katika pango la Hiraa´ na akamwambia: “Soma!” Akasema: “Mimi si mwenye kusoma.” Akimaanisha kwamba hajui kusoma. Akamkamata mkamato wa nguvu kisha akamwacha na kumwambia: “Soma!” Akasema: “Mimi si mwenye kusoma.” Akamkamata mkamato wa nguvu kisha akamwacha na kumwambia: “Soma!” Akasema: “Mimi si mwenye kusoma.” Akamwambia:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ

“Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba – amemuumba mtu kutokana na pande la damu linaloning’inia!”[1]

Hivi ndivo ilivyokuwa unabii wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah alimfanya kuwa Nabii kwa njia hiyo. Kisha akaenda nyumbani hali ya kutetemeka kwa khofu. Kwa sababu amekutana na kitu ambacho hakuwa anakijua hapo kabla. Inahusiana na jambo kubwa. Akamkuta mke wake Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambapo akamfunika na kumtuliza na akamwambia: “Hapana! Ninaapa kwa Allaah kwamba Allaah hatokufedhehesha. Kwani wewe unawaunga jamaa, unamwangalia dhaifu na ni mwenye kusimama nyuma ya haki.”

Akamtuliza na akaenda naye kwa ami yake Waraqah bin Nawfal. Alikuwa ni mfanya ´ibaadah na amesoma vitabu vya kale kwa ajili ya kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall). Akamweleza aliyoyaona ambapo akamwambia:

“Hii ni Naamuus iliyokuwa ikiteremka kwa Muusa.”

Bi maana ni Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 96:01-02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 247-249
  • Imechapishwa: 04/02/2021