122. Kuzaliwa kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Kuhusu kuzaliwa kwake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizaliwa mwaka wa ndovu. Huo ni ule mwaka alipokuja mfalme Abrahah ambaye alikuwa mfalme wa Yemen. Mfalme wa Uhabeshi alimwagiza akaibomoe Ka´bah akiwa na ndovu mkubwa. Walipofika sehemu inayoitwa “al-Mughammas” na hakuna kilichobaki isipokuwa tu kuingia Makkah na kuibomoa Ka´bah. Wakati huo wakazi wa Makkah wametawanyika na kupanda milima kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kupambana nao. Walipotaka kuielekea Ka´bah, ndovu ikajizuia na ikakataa kusimama kutoka ardhini. Allaah ndiye alimzuia. Anapoelekea upande usiokuwa Makkah anasimama na kukimbia. Anapoelekezwa upande wa Makkah anajizuia na anashindwa kutembea. Walipokuwa katika hali hiyo wakaona mtawanyiko wa ndege kutokea upande wa baharini wakiwa na mawe. Kila ndege alikuwa na mawe mawili, jiwe moja mdomoni mwake na jiwe jengine miguuni mwake. Wakirusha vile vijiwe na ikawa vijiwe hivyo vinampata mtu kichwani mwake. Jiwe hilo linatokea katika tupu yake ya nyuma na anapasuka vipande viwili. Ndipo Allaah akawaangamiza. Allaah akateremsha juu ya tukio hilo Suurah “al-Fiyl” akiwakumbusha Quraysh:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ

“Je, hukuona jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wa ndovu? Je, hakufanya vitimbi vyao katika maangamizi? Na akawatumia juu yao ndege makundi kwa makundi? Wakiwarushia mawe ya udongo uliookwa motoni.”

Kutokea Jahannam.

فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ

“Akawafanya kama majani yaliyoliwa.”[1]

Wakawa kama nyasi zilizoliwa na mnyama kisha akayatema.

Hiki ndio kisa cha ndovu. Allaah akaihami nyumba Yake tukufu na akamwangamiza mjeuri huyu. Katika mwaka huu ndio alizaliwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kulionekana miujiza wakati wa kuzaliwa kwake. Kulidhihiri pamoja naye nuru iliyoangaza majumba ya Shaam. Wakati wa kuzaliwa kwake masanamu yalitetemeka, Iywaan wa kisraa akatetemeka na waheshimiwa wote wakaanguka katika usiku wa kuzaliwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huu ulikuwa ni msingi wa kutumilizwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Majini na mashaytwaan wakapatwa na ukelele katika usiku huu mtukufu.

Alizaliwa mahali kunakoitwa Sha´ab karibu na Ka´bah. Alizaliwa Makkah. Lakini hakuna ulengeshaji uliyothibiti wa maeneo ya nyumba.

[1] 105:01-05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 246-247
  • Imechapishwa: 04/02/2021