122. Aina ya pili ya waislamu kuwafanya makafiri marafiki na vipenzi

2- Fungu la pili: Akawasaidia dhidi ya waislamu kwa kulazimishwa na si kwa kutaka kwake mwenyewe, wakati huohuo hawapendi, bali amelazimishwa juu ya hilo kwa sababu anaishi kati yao. Mtu kama huyu ana matishio makali na anakhofiwa juu yake kufuru inayomtoa katika Uislamu. Hilo ni kwa kuwa washirikina walipowalazimisha kundi katika waislamu siku ya Badr kutoka pamoja nao kuwapiga vita waislamu, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) aliwakaripia kitendo hicho kwa vile waliacha Hijrah na wakabaki pamoja na washirikina na wakazitia nafsi zao wenyewe katika yale waliyotumbukia ndani yake ambapo walilazimishwa kutoka bega kwa bega pamoja nao, licha ya kwamba wanachukia dini ya makafiri na wanapenda dini ya waislamu, lakini walibaki Makkah kwa kushughulishwa na mali zao, mji wao na watoto wao[1], na si kwa ajili ya kuwapenda makafiri au kupenda dini yao. Ndipo Allaah akateremsha (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ

”Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali wamejidhulumu nafsi zao, [Malaika] watawaambia: “Mlikuwa katika hali gani?”

Bi maana mlikuwa pamoja na kundi gani? Haya ni makemeo. Kwa msemo mwingine ni kama vile wanaulizwa ni kwa nini walikuwa pamoja na washirikina ilihali nyinyi ni waislamu?

قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ

“Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.”

Bi maana hatukuwa na namna. Wao ndio wametulazimisha katika jambo hilo.

قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا

“Watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahajiri humo?”

Kwa nini mvumilie kubaki pamoja na makafiri na nyinyi ni waislamu na mkaziweka nafsi zenu katika mliyotumbukia ndani yake?

فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Basi hao makazi yao yatakuwa ni [Moto wa] Jahannam – na ubaya ulioje mahali pa kurejea!”

Haya ni matishio makali kwao.

إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ

”Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao hawakuweza kupata namna yoyote ile wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao huenda Allaah akawasamehe.” (an-Nisaa´ 04:98-99)

Yule mwenye kuacha Hijrah naye anaweza na wala asihame na akabaki anaishi pamoja na washirikina, na baya zaidi kuliko hilo, ni kwamba wakamtoa pamoja nao ili kuwapiga vita waislamu, huyu ana matishio makali. Ama yule ambaye ameacha kufanya Hijrah kwa kuwa hakuweza, basi Allaah amesema:

إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ

”Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto…”

Watu hawa ni wenye kupewa udhuru kwa kule kubaki kwao kwa sababu hawawezi kufanya Hijrah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa vile inavoweza.” (al-Baqarah 02:286)

[1] al-Bukhaariy (3596), Ibn Jariyr (05/274-275) na al-Baghawiy (01/369).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 159-160
  • Imechapishwa: 19/02/2019