120. Majina ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Alikuwa ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim. Haashim alikuwa anatokamana na [kabila la] Quraysh, Quraysh ni kutokamana na waarabu na waarabu ni kutokamana na kizazi cha Ismaa´iyl, mtoto wa Ibraahiym al-Khaliyl – baraka za juu na salaam ziwe juu yake na kwa Mtume wetu.

MAELEZO

 Hili ndio jina lake na nasaba yake. Jina lake ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ana majina mengine mbali na Muhammad. Lakini jina lililotangaa zaidi ni Muhammad. Allaah ameyataja hayo katika Qur-aan katika Aayah nyingi:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah.”[1]

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ

“Muhammad si chochote isipokuwa ni Mtume tu [na] wamekwishapita kabla yake Mitume [wengine].”[2]

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu…”[3]

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَآمَنُوا بِمَا نُزِّلَ عَلَىٰ مُحَمَّدٍ وَهُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ

”Wale walioamini na wakatenda mema na wakaamini yale aliyoteremshiwa Muhammad, nayo ni ya haki kutoka kwa Mola wake.”[4]

Hivyo Allaah akataja jina lake la Muhammad katika Aayah nyingi.

Miongoni mwa majina yake ni Ahmad. Allaah amelitaja katika maneno Yake katika bishara ya al-Masiyh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُم مُّصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ

“Na kumbuka wakati ´Iysaa mwana wa Maryam aliposema: “Enyi wana wa Israaiyl! Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu mwenye kusadikisha yaliyo kabla yangu katika Tawraat na mwenye kubashiria kuja kwa Mtume baada yangu jina lake Ahmad.”[5]

Yeye ni Ahmad na Muhammad. Maana yake ni mwenye kusifiwa sana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mwenye sifa nyingi anazosifiwa kwazo.

Miongoni mwa majina yake ni Mtume wa huruma na Mtume wa al-Malhamal ikiwa na maana ya jihaad katika njia ya Allaah, Haashir na al-´Aaqib (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye aliwakusanya watu baada ya kutumilizwa kwake kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye alikuwa Mtume wa mwisho. Hakuna baada yake isipokuwa kusimama kwa Qiyaamah na watakusanywa watu kwa ajili ya malipo na hesabu. Anayetaka kuyajua mambo haya basi arejee katika kitabu “Jalaal-ul-Afhaam fiys-Swalaatu was-Salaam ´alaa khayr-il-Anaam” cha Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah).

[1] 48:29

[2] 03:144

[3] 33:40

[4] 47:02

[5] 61:06

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 243-244
  • Imechapishwa: 03/02/2021