12. Watu waliopinda kutokamana na ´Aqiydah sahihi

Kuna sampuli mbalimbali za watu waliopinda kutokamana na ´Aqiydah hii na wakafuata yale yenye kupingana nayo. Miongoni mwao kuko wenye kuabudia masanamu, mizimu, Malaika, mawalii, majini, miti, mawe na vinginevyo. Watu hawa hawakuitikia ulinganizi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Bali wameenda kinyume nao na wakakaidi. Hivyo ndivyo Quraysh na makabila mengine ya kiarabu walivyomfanyia Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Watu hawa walikuwa wakiwaomba waungu wao wawatatulie haja zao, wawaponye maradhi na wawanusuru dhidi ya maadui wao. Vilevile walikuwa wakiwachinjia na wakiwawekea nadhiri. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowakemea kufanya hivo na badala yake akawaamrisha wamtakasie ´ibaadah Allaah peke yake, walishangzwa na hilo na wakamkemea hali ya kusema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖإِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu wote hawa kuwa ni mungu Mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (38:05)

Hata hivyo hakuacha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalingania katika dini ya Allaah na wakati huohuo akiwatahadharisha shirki na akiwawekea wazi uhakika wa yale anayowalingania kwayo mpaka Allaah akawaongoza katika wao aliwaongoza. Baada ya hapo wakaingia katika dini ya Allaah makundi kwa makundi. Hatimaye dini ya Allaah ikazishinda dini zingine baada ya ulinganizi wenye kuendelea na mapambano marefu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na wale waliowafuata kwa wema. Baada ya hapo mambo yakabadilika na ujinga ukawa mwingi kwa watu mpaka wengi wakarudi katika dini ya kipindi cha kishirikina kwa kupetuka mipaka kwa Mitume, mawalii, kuwaomba du´aa, kuwataka uokozi na aina nyenginezo za shirki. Hawakuelewa maana ya “Laa ilaaha illa Allaah” kama walivyoelewa maana yake makafiri wa kiarabu. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada. Mpaka hii leo watu hawajaacha kuwa na shirki kama hii kutokana na sababu ya kuwa na ujinga mwingi na kuwa mbali na zama za utume.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 31/05/2023