Usiku na mchana ni sehemu tukufu ya kuchuma kwa yule ambaye atavitumia katika kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Pahali pa kufanya matendo ni usiku na mchana. Huna zaidi ya usiku na mchana. Ni sehemu ya matendo na kuchuma chumo zuri kwa ajili ya dunia na Aakhirah.  Allaah ameapa kwa alasiri kutokana na mazingatio na faida zinazopatikana katika jambo hilo. Jawabu la kiapo ni nini? Ni maneno Yake:

إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْر

“Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara.”

Watu ni wanaadamu wote. Hakumvua yeyote; si wafalme, maraisi, matajiri, mafukara, waungwana, watumwa, waume kwa wake. Hapa inahusu wanaadamu wote wamo khasarani. Kwa msemo mwingine wamo katika khasara na maangamivu wakipoteza wakati huu wenye thamani na wakautumia katika kumuasi Allaah na katika mambo yanayowadhuru.

Wakati huu ndio kitu duni sana kwa watu wengi. Unawarefukia wakati wakichoka na wakisema kuwa wanataka kuua wakati ambapo wanafanya mambo ya pumbao, wanasafiri kwenda katika nchi za nje wakati wa likizo zao au utawaona wakicheka na wakifanya utani kwa ajili ya kukata wakati. Watu hawa ambao wanaukata wakati na kuupoteza utakuja kuwa khasara na majuto kwao siku ya Qiyaamah. Wakati ndio chanzo cha kufaulu kwao iwapo wangeulinda. Wanaadamu wote wako katika khasara na katika maangamivu. Isipokuwa wale wenye kusifika kwa sifa nne; elimu, matendo, kulingania kwa Allaah na kufanya subira juu ya maudhi. Yule mwenye kusifika kwa sifa hizi nne basi ataokoka kutokamana na khasara hii. Haiyumkiniki kumwamini Allaah isipokuwa kwa ujuzi ambao ndio kumtambua Allaah. Maneno Yake:

وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ

“… wakatenda mema.”

Bi maana wakafanya matendo mema katika mambo ya wajibu na yaliyopendekezwa. Kwa msemo mwingine ni kwamba wametumia wakati wao kwa kufanya matendo mema katika yale yanayowanufaisha katika dini na dunia yao. Hata kufanya kazi ya kidunia ndani yake mna kheri na thawabu endapo mtu kwa kufanya hivo atakusudia imsaidie kumtii Allaah. Ni vipi ikiwa mtu atafanya matendo kwa ajili ya Aakhirah? Muhimu ni kwamba wewe usipoteze wakati wako. Utumie wakati wako katika kitu kinachokunufaisha.

Maneno Yake:

وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ

“… wakausiana kwa kufuata ya haki… “

Wakaamrishana mema na kukatazana maovu na wakalingania kwa Allaah (´Azza wa Jall), wakafundisha elimu yenye mnufaa, wakaeneza elimu na kheri kati ya watu na wakawa ni walinganizi kwa Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 25/11/2020