12. Ubainifu wa ni nani mwanachuoni na wenye kujifananisha nao


Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa nne:

Kubainisha elimu na wanazuoni, Fiqh na wanazuoni wa Fiqh [Fuqahaa´], na ubainifu wa yule mwenye kujifananisha na wao ilihali si katika wao. Allaah (Ta´ala) amebainisha msingi huu mwanzoni wa Suurah “al-Baqarah” kutoka katika maneno Yake:

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ

“Enyi wana wa Israaiyl! Kumbukeni neema Yangu Niliyokuneemesheni…”[1]

Mpaka katika Kauli Yake kabla ya kutaja Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Enyi wana wa Israaiyl! Kumbukeni neema Yangu Niliyokuneemesheni na hakika Mimi Nimekufadhilisheni juu ya walimwengu.”[2]

Hilo linazidi zaidi kuwa wazi na yale yaliyosemwa wazi wazi na Sunnah katika maneno haya mengi yaliyo wazi kwa mjinga aliye mpumbavu.

Kisha ikawa jambo hili ni katika mambo mageni zaidi na ikawa elimu na Fiqh ndio Bid´ah na upotevu na bora walilo nalo wao ni kuchanganya haki na batili. Ikawa elimu ambayo Allaah (Ta´ala) ameifaradhisha juu ya viumbe na akaisifia hakuna mwenye kuitamka isipokuwa zindiki na mwendawazimu. Na akawa yule mwenye kuipinga na kuifanyia uadui na akaandika kutahadharisha na kukataza [juu ya mtu wa elimu] ndio msomi na mwanachuoni.

MAELEZO

Kubainisha elimu… – Makusudio ya ´elimu` hapa ni elimu ya dini. Ni ile elimu ambayo Allaah amemteremshia Mtume Wake katika mabainisho na uongofu. Elimu ambayo kuna kusifiwa ni ile elimu ya Shari´ah; elimu ambayo Allaah amemteremshia Mtume Wake  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua? Hakika si venginevyo wanakumbuka wenye akili tu.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa ufahamu katika dini.”[4]

“Hakika Mitume hawarithiwi dinari wala dirhamu. Lakini si vyenginevyo wanachorithiwa ni elimu. Hivyo basi yule mwenye kuinyakua basi amejinyakulia fungu kubwa.”[5]

Ni jambo linalotambulika kwamba elimu waliyorithiwa wanachuoni ni elimu ya Shari´ah. Hata hivyo sisi hatupingi kuwa kuna faida katika elimu nyenginezo. Lakini ni faida yenye pande mbili; ikisaidia juu ya kumtii Allaah, kunusuru dini ya Allaah na wakanufaika kwayo waja wa Allaah basi inakuwa ni kheri na manufaa.

Baadhi ya wanachuoni wametaja kwamba kujifunza mambo ya tasnia ni faradhi kwa baadhi ya watu, jambo ambalo lina lina mvutano na lina walakini. Kwa hali yoyote elimu ambayo kumepokelewa kusifiwa watu wake na wale wenye kuitafuta ni elimu ya Qur-aan na Sunnah. Elimu nyenginezo, ikiwa ni njia inayopelekea katika kheri basi ni kheri, na ikiwa ni njia inayopelekea katika shari basi ni shari. Vinginevyo ni kupoteza wakati na upuuzi mtupu.

[1] 02:40

[2] 02:122

[3] 39:09

[4] al-Bukhaariy (71) na Muslim (1923).

[5] at-Tirmidhiy (2691), Abu Daawuud (3641) na Ibn Maajah (223). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Ibn Maajah” (182).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 22/06/2021