Hayo nimeyaandika miaka kumi iliyopita kama utangulizi wa kitabu hiki. Hivi sasa imedhihiri kwamba ni jambo lina taathira nzuri katika safu ya waumini vijana kwa vile wameongozwa katika kuiasisi dini na ´ibaadah zao katika chemchem safi; Qur-aan na Sunnah. Vijana sampuli hii wamezidi kuwa wengi ambao wameanza kuitendea kazi Sunnah na kuabudu kwayo, mpaka wamekuwa ni wenye kutambulika kwa jambo hilo. Sio kwa sababu wana mashaka juu ya uwajibu wake, isipokuwa ni kwa sababu ya mashaka kutoka kwa wale wenye kufuata kichwa mchunga. Kwa ajili hiyo ndio maana nataka kuzitaja shubuha hizo na kuziraddi ili waanze kuitendea kazi Sunnah pamoja na wale wengine wenye kufanya hivo na wawe – kwa idhini ya Allaah – miongoni mwa lile kundi lililookoka.

Shubuha ya kwanza: Baadhi wanasema kwamba ni wajibu kuyarudisha mambo ya dini yetu katika uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), khaswakhaswa katika yale mambo yanayohusiana na ´ibaadah safi isiyokubali maoni na Ijtihaad kutoka kwa mtu, kama mfano wa swalah, kwani ´ibaadah imejengeka juu ya Qur-aan na Sunnah peke yake. Hata hivyo hatuna wanachuoni wenye kufuata kipofu ambao wanaamrisha jambo hilo. Bali tunaona kuwa wanakubali mambo ya tofauti na wanamaanisha kuwa ni kuwafanyia wepesi Ummah. Wanatumia hoja kwa Hadiyth isemayo:

“Kutofautiana kwa Ummah wangu ni rehema.”

Inaonekana kuwa Hadiyth hii inaenda kinyume na ule mfumo ambao wewe unalingania kwao na umetunga kitabu chako hiki na vyengine juu yake. Unasemaje juu ya Hadiyth hii?

Mosi ni kwamba Hadiyth si Swahiyh. Ni batili na haina msingi wowote. ´Allaamah as-Subkiy amesema:

“Sijapata juu yake cheni ya wapokezi Swahiyh, dhaifu wala iliyozuliwa.”

Hata hivyo imepokelewa kwa tamko:

“Kutofautiana kwa Maswahabah wangu ni rehema juu yenu.”

na:

“Maswahabah zangu ni kama nyota; yoyote mtakayemfuata mmeongoka.”

Hakuna yoyote katika hizo iliyosihi. Ya kwanza ni dhaifu sana, kama nilivyohakiki katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah”[1].

Pili ni kwamba inaenda kinyume na Qur-aan tukufu ambayo inakataza kutofautiana katika dini na inaamrisha kuwa na umoja katika dini. Kwa mfano Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ ۖ وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Na mtiini Allaah na Mtume wake na wala msizozane, mtavunjika moyo na zikatoweka nguvu zenu na subirini. Hakika Allaah yupamoja na wenye kusubiri.”[2]

وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُشْرِكِينَ مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“… na wala msiwe miongoni mwa washirikina; miongoni mwa wale walioifarikisha dini yao wakawa makundimakundi – kila kundi wananafurahia waliyonayo.”[3]

وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ

“Na hawatoacha kuendelea kutofautiana. Isipokuwa yule aliyemrehemu Mola wako.”[4]

Ikiwa wale waliorehemewa na Mola wako hawatofautiani; isipokuwa tu watu wa batili ndio wenye kutofautiana. Ni vipi basi itaingia akilini kwamba tofauti iwe ndio rehema? Hivyo ikathibiti kuwa Hadiyth hii si Swahiyh, si katika cheni ya wapokezi wala kimaana[5]. Hapo ndipo itabainika kwamba haifai kuitumia kwa ajili ya kukwepa kuitendea kazi Qur-aan na Sunnah, jambo ambalo limeamrishwa na maimamu.

[1] Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah (58, 59 na 61).

[2] 08:46

[3] 30:31-32

[4] 11:118-119

[5] Yule anayetaka kujua kwa undani basi arejee katika marejeo yaliyotangulia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 52-53