47- Halafu ataenda katika Swafaa na Mawrah ili aweze kufanya Sa´y baina yake. Atapokurubia basi atasoma maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللّهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ

“Hakika vilima vya Swafaa na Marwah ni katika alama za Allaah. Basi anayehiji katika Nyumba hiyo au akafanya ´Umrah, si kosa kwake kuvizunguka. Na anayejitendea mwenyewe kheri, basi bila ya shaka Allaah ni Mwenye shukrani na Mjuzi.”[1]

Halafu atasema:

نبدأ بما بدأ الله به

“Tunaanza kwa kile alichoanza nacho Allaah.”

48- Halafu ataanzia Swafaa na atapanda juu yake mpaka aweze kuiona Ka´bah[2].

49- Hivyo aielekee Ka´bah, ampwekeshe Allaah na aseme:

الله أكبر الله أكبر الله أكبر

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد يحيي ويميت وهو على كل شيء قدير،

لا إله إلا الله وحده لا شريك له أنجز وعده ونصر عبده وهزم الأحزاب وحده

“Allaah ni mkubwa. Allaah ni mkubwa. Allaah ni mkubwa. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye. Anahuisha na Anafisha. Naye juu ya kila jambo ni muweza. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ameitimiza ahadi Yake, amemnusuru mja Wake na amevishinda vikosi hali ya kuwa peke yake.”[3]

Atayasema haya mara tatu. Ataomba kati ya hayo[4].

50- Kisha atateremka afanye Sa´y kati ya Swafaa na Marwah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni Sa´y. Kwani hakika Allaah amewafaradishia kufanya Sa´y.”[5]

51- Baada ya hapo atatembea mpaka ile sehemu yenye alama [mataa ya kijani] upande wa taakulia na upande wa kushoto. Atapofika pale, basi atatakiwa kutembea kwa haraka  mpaka katika alama nyingine. Zama zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni bonde ilio wazi ndani yake kuna changarawe. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Bonde halivukwi isipokuwa kwa mwendo wa kasi.”[6]

Halafu atatembea hali ya kupanda juu mpaka atafika katika Marwah na atapanda juu yake. Hapo atafanya yaleyale aliyofanya Swafaa katika kuelekea Qiblah, kusema “Allaahu Akbar”, “Laa ilaaha illa Allaah” na du´aa[7].  Huu ni mzunguko mmoja.

52- Atatembea mahali pa kutembea kwake na atakwenda haraka mahali pa kwenda haraka mpaka pale atapopanda Swafaa. Huu ni mzunguko wa pili.

53- Kisha arudi Marwah na vivyo hivyo mpaka atakapokamilisha mizunguko saba na ukomo wa mwisho wake ni kwenye Marwah.

54- Inajuzu kwake kutukufu kati ya Swafaa na Marwah hali ya kuwa ni mwenye kupanda. Kwa upande mwingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amependeza zaidi kutembea kwa miguu[8].

55- Akiomba katika Sa´y kwa kusema:

رب اغفر وارحم إنك أنت الأعز الأكرم فلا بأس لثبوته عن جمع من السلف

“Ee Allaah! Nisamehe na unirehemu. Kwani hakika Wewe ni Mtukufu zaidi, Mwenye kushinda zaidi.”

hapana neno. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa kundi katika Salaf[9].

56- Atapofika wa mzunguko wa saba na akafika Marwah, atafupisha nywele za kichwa chake[10]. Kwa hivo atakuwa amefanya ´Umrah. Kitakuwa halali kwake kile kilichokuwa haramu kwa sababu ya Ihraam. Atabaki katika hali hiyo hali ya kuwa ni mwenye kutoka Ihraam mpaka siku ya Tarwiyah.

57- Yule aliyekuwa amehirimia pasi na ´Umrah ya hajj na akawa hakukokota mnyama kutokea nje ya Haram, basi ni wajibu kwake kutoka kwenye Ihraam kwa ajili ya kufuata maamrisho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kujikinga na ghadhabu zake. Ama kuhusu yule aliyekokota mnyama, ataendelea katika Ihraam yake na wala hatotoka katika Ihraam isipokuwa baada ya kutupa mawe ile siku ya kuchinja.

[1] 02:158

[2] Leo si jambo jepesi kuiona Ka´bah isipokuwa katika baadhi ya maeneo katika Swafaa. Mtu anaweza kuiona kupitia nguzo ambazo zimejengwa juu yake katika ghorofa ya pili katika msikiti. Mwenye kuweza kufanya hivo, basi ameisibu Sunnah. Asipoweza kufanya hivo, afanye awezacho na hakuna neno.

[3] Ameongeze katika “al-Adhkaar” “Laa ilaaha illa Allah wa laa na´bud illa Iyyaah… ” Sijaiona nyongeza hii katika njia za Hadiyth kwa Muslim wala kwa mwingine ambaye ameipokea kutoka katika Hadiyth ndefu ya Jaabir. Hili ni tofauti na yale ambayo mtu anaweza kufikiria kutoka katika taaliki yake inayosema:

“Ameipokea Muslim na… “

[4] Bi maana ataomba kwa akitakacho kati ya Tahliylaat kwa kile ambacho ndani yake mna kheri za duniani na Aakhirah. Hata hivyo lililo bora ni kuomba du´aa ambayo imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au as-Salaaf as-Swaalih.

[5] Hadiyth hii ni Swahiyh, tofauti na vile walivosema baadhi yao. Imetajwa katika “al-Irwaa´” (1072).

[6] Ameipokea an-Nasaa´iy na wengineo. Imetajwa katika ”al-Hajj al-Kabiyr”.

Faida! Ibn Qudaamah amesema katika “al-Mughniy”:

“Twawaaf ya wanawake na Sa´y yao ni kwa kutembea njia nzima. Ibn-ul-Mundhir amesema: “Wanachuoni wameafikiana juu ya kwamba wanawake hawatakiwi kwenda kwa mwendo wa kasi kuizunguka Nyumba wala kati ya Swafaa na Marwah. Wala hawatakiwi kupitisha nguo yao chini ya kwapa. Hayo ni kwa sababu msingi ni kwamba kitendo hichi kinafanywa kwa sababu ya kudhihirisha ngozi, jambo ambalo hawakusudiwi wanawake. Lengo kwa mwanamke ni yeye kujisitiri ilihali kwenda mwendo wa kasi na kupitisha nguo chini ya kwapa kunapingana waziwazi kabisa na jambo hilo.”

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” jambo ambalo linafahamisha kwamba masuala haya Shaafi´iyyah wametofautiana. Amesema:

“Kuna maoni mawili:

1- Hatakiwi kwenda mwendo wa kasi. Badala yake anatakiwa kutembea njia nzima sawa iwe ni mchana au usiku. Haya ndio maoni sahihi na ndio maoni ya wengi.

2- Akiweza kwenda harakaharaka usiku, wakati ambapo hakuna mtu mahala hapo, basi itakuwa imependekezwa kwake kama wanaume.” (08/75)

Inawezekana haya ndio yakawa karibu zaidi na usawa. Kwani msingi wa kwenda haraka ilikuwa pindi mama yake na Ismaa´iyl Haajar alipokimbia wakati alipokuwa anamtafutia maji mwana wake aliyekuwa na kiu. Kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas:

“Akakuta Swafaa ndio mlima ulio karibu zaidi na yeye. Kisha akasimama juu yake na kulielekea bonde kutazama kama ataweza kumuona yeyote. Hakuweza kumwona yeyote. Ndipo akateremka kutoka Swafaa mpaka alipofika kwenye bonde, ndipo akanyanyua ncha ya kishale (shuka ya juu) na akaanza kwenda haraka mpaka alipopita bonde lote na akafika kwenye Marwah. Kisha akasimama juu yake na kulielekea bonde kutazama kama ataweza kumuona yeyote. Hakuweza kumwona yeyote. Alifanya hivo mara saba.”

Ibn ´Abbaas ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hiyo ndio Sa´y ya watu baina yazo (Swafaa na Marwah).” (Ameipokea al-Bukhaariy katika mlango ”al-Anbiyaa’”)

[7] Ama kuiona Ka´bah sasa hivi haiwezekani kwa sababu ya kuzuia jengo baina yake. Kwa hivyo mtu ajitahidi kuielekea. Asifanye kama yale yanayofanywa na watu waliodangana ambao hunyanyua macho yao na mikono yao kuelekeza mbinguni.

[8] Ameipokea Abu Nu´aym katika “Mustakhraj Swahiyh Muslim”.

[9] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (4/68-69) kwa sanadi mbili Swahiyh kutoka kwa Ibn Mas´uud na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Musayyab bin Raafiy´ al-Kaahiliy na ´Urwah bin az-Zubayr. Vilevile imepokelewa na at-Twabaraaniy kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa cheni ya wapokezi dhaifu, kama ilivyotajwa katika ”al-Majma´” (3/248).

[10] Ikiwa baina ya ´Umrah na hajj yake kuna muda mrefu unaotosheleza nywele kurefuka, basi anaweza kunyoa nywele zake.” (Rejea katika ”Fath-ul-Baariy” (3/444))

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 15/07/2018