[20] Ana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alama kubwa za ardhini na mbinguni. Hakuna mtu mwingine anayeshirikiana naye kwazo wala kuzifikia. Mtu mwenye busara na mwenye uoni wa mbali akizizingatia, basi atatambua kuwa Allaah amemtunuku nafasi na ngazi tukufu na akamfadhilisha kwazo juu ya walimwengu wengine wote. Alama hiyo ni kwamba usiku mmoja alimpanda mnyama al-Buraq kumpeleka Yerusalemu. Halafu akanyanyuliwa juu mbinguni ambapo akawasalimia Malaika na Mitume ambao pia aliwaswalisha. Aliingia Peponi na akauona Moto. Katika usiku huo akafaradhishiwa swalah na akamuona Mola Wake. Akasogea karibu Naye na akazungumza Naye na akamtukuza. Akaona karama na alama. Akamsogelea Mola Wake na akawa kiasi cha umbali wa mipinde miwili au karibu zaidi. Allaah aliuweka mkono Wake juu ya mabega yake na akahisi ubaridi kati ya matiti yake na akapata elimu za wale wa mwanzo na wa mwisho. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ

“Hatukuijaalia ndoto ambayo tulikuonyesha isipokuwa ni [kutaka kuwatia] mtihani kwa watu.”[1]

Uonaji huu ulitokea katika hali ya umacho na haikuwa ndoto. Usiku huohuo akarudi kwa mwili wake kwenda Makkah. Akaeleza kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) huko Aakhirah atapewa fadhilah na utukufu zaidi kuliko alivyopewa hapa duniani na akasema:

وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضَىٰ

“Bila shaka Mola wako atakupa na utaridhika.”[2]

[1] 17:60

[2] 93:05

  • Mhusika: Imaam Abul-Husayn Muhammad bin Abiy Ya´laa al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-I´tiqaad, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 26/02/2019