12. Safari inafungwa kwa ajili ya msikiti wake na si kaburi lake

Swali: Ni ipi hukumu ya kusafiri kwa ajili ya kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mengineyo katika makaburi ya mawalii na waja wema?

Jibu: Haijuzu kusafiri kwa lengo la kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kaburi la mtu mwengine kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kusifungwe safari isipokuwa kuelekea katika misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti huu na msikiti wa al-Aqswaa.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Kilichowekwa katika Shari´ah kwa ambaye anataka kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali yuko mbali na Madiynah akusudie kuutembelea msikiti wake na hivyo kaburi lake tukufu, kaburi la Abu Bakr, ´Umar na mashahidi wa al-Baqiy´ yatafuatia jambo hilo.

Itafaa pia akinuia tangu mwanzo. Kwa sababu inafaa katika hali ya kufuatia yale yasiyojuzu katika hali ya kujitegemea. Ama kunuia kulitembelea kaburi peke yake haijuzu ikiambatana na kufunga safari. Lakini ikiwa ni karibu na wala hahitaji kufunga safari na kule kwenda kwake hakuitwi kuwa ni safari basi hapana neno kufanya hivo. Kwa sababu kulitembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makaburi ya marafiki zake bila kufunga safari ni imependekezwa na ni kujikurubisha kwa Allaah. Hukumu hiyohiyo juu ya kuyatembelea makaburi ya mashahidi wa al-Baqiy´ na makaburi ya waislamu kila mahali imependekezwa na ni kujikurubisha kwa Allaah. Lakini ifanyike pasi na kufunga safari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwafunza Maswahabah zake wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”[3]

Ameipokea pia Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

[1] al-Bukhaariy (1864) na Muslim (1397).

[2] Muslim (976).

[3] Muslim (974).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 21/04/2022