[19] Miongoni mwa hayo ni kitabu chake ambacho kinavihukumu vitabu vyengine vyote na kinachovitolea khabari, kinachovitolea ushahidi na kuvisadikisha. Hakifanani na mashairi wala barua. Kimetakasika na maneno mengine yote. Kimefazaisha usikizi na uelewa. Hakiingiliwi na batili mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mwenye kustahiki kuhimidiwa. Watu na majini wameshindwa kuleta mfano wake, japokuwa watakuwa ni wenye kusaidizana wao kwa wao. Ni kitabu kilichokusanya mifumo, miujiza, ufafanuzi, ufaswaha, balagha, matahadharisho, mawaidha, maamrisho kuhusu kila utiifu, karama, adabu, makatazo kuhusu kila uovu na aina zote kubwa za ´ibaadah kama twahara, swalah, swawm, zakaah, hajj, jihaad, kuunga udugu, kujitolea, zawadi, swadaqah, utimizaji, kuogopa, kutaraji na aina nyenginezo zisizohesabika. Wakati watu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walipomwambia:

ائْتِ بِقُرْآنٍ غَيْرِ هَـٰذَا أَوْ بَدِّلْهُ

“Lete Qur-aan nyingine badala ya hii au ibadilishe.”

akasema:

مَا يَكُونُ لِي أَنْ أُبَدِّلَهُ مِن تِلْقَاءِ نَفْسِي ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ

“Hainipasii mimi kuibadilisha kwa khiyari ya nafsi yangu. Mimi sifuati isipokuwa tu yale nilofunuliwa Wahy.”[1]

Bi maana kutoka kwa Mola wangu. Halafu akawaambia:

لَّوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا تَلَوْتُهُ عَلَيْكُمْ وَلَا أَدْرَاكُم بِهِ ۖ فَقَدْ لَبِثْتُ فِيكُمْ عُمُرًا مِّن قَبْلِهِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

“Kama angetaka Allaah nisingelikusomeeni na wala asingelikujulisheni nayo. Kwani nimekwishaishi nanyi umri wote kabla yake.  Je, basi hamfahamu?”[2]

Bi maana kwa miaka arubaini mimi ni yatima, fakiri, si mwenye kujua kusoma wala kuandika, sikuwa naenda kwa mwalimu wowote, mchawi, kuhani wala mshairi. Je, hivi si mzingatie hayo? Mnajua fika ya kwamba Aayah mfano wa hizi hakuna aziwezaye isipokuwa Allaah – hamkuweza kufanya hivo na wala hamtoweza kufanya hivo.

Akafanya Aayah hizi ni zenye kushinda katika uhai wake na baada ya kufa kwake pasi na yeyote kuja na mfano wake. Hakuna yeyote aliyefanikiwa kuja na mfano wa Qur-aan kwa upande wa Aayah zake, mpangilio wake, ukweli wake, usahihi wa maana yake na elimu zake kubwa. Kadhalika viumbe hawakuweza kuzunguka uelewa wake wala kufikia kilele cha elimu yake. Isitoshe yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekhabarisha kuhusu watu wa kale na wataokuja nyuma:

غُلِبَتِ الرُّومُ فِي أَدْنَى الْأَرْضِ وَهُم مِّن بَعْدِ غَلَبِهِمْ سَيَغْلِبُونَ فِي بِضْعِ سِنِينَ

“Warumi wameshindwa. Katika nchi iliyo karibu, nao baada ya kushindwa kwao watashinda hivi karibuni. Katika miaka michache.”[3]

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ

“Utashindwa mjumuiko wao na watageuza migongo.”[4]

Ameelezea hayo kabla ya kutokea kwake. Amesema (Ta´ala):

تِلْكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهَا إِلَيْكَ ۖ مَا كُنتَ تَعْلَمُهَا أَنتَ وَلَا قَوْمُكَ مِن قَبْلِ هَـٰذَا

“Hizo ni katika khabari zilizofichikana Tunazokufunulia Wahy. Hukuwa unazijua wewe na wala watu wako kabla ya hii [Qur-aan].”[5]

[1] 10:15

[2] 10:16

[3] 30:02-04

[4] 54:45

[5] 11:49

  • Mhusika: Imaam Abul-Husayn Muhammad bin Abiy Ya´laa al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-I´tiqaad, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 26/02/2019