12. Mwenye kuona kuwa kuna uongofu au hukumu bora zaidi kuliko ya Mtume

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

04 – Mwenye kuamini kuwa kuna uongofu usiokuwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni mkamilifu zaidi kuliko uongofu wake au kuna hukumu ya myingine asiyekuwa yeye ilio bora zaidi kuliko hukumu yake. Ni kama mfano wale wenye kufadhilisha hukumu za Twawaaghiyt juu ya hukumu yake. Huyo ni kafiri.

MAELEZO

Kichenguzi cha nne kinachochengua Uislamu ni kwamba yule mwenye kuamini kuwa kuna uongofu mkamilifu zaidi usiokuwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kwamba kuna hukumu bora zaidi isiyokuwa hukumu yake amekufuru kwa maafikiano. Kwa mfano wale wenye kufadhilisha hukumu za Twawaaghiyt juu ya hukumu ya Allaah na Mtume Wake. Mwenye kuitakidi kuwa kuna uongofu ulio mkamilifu zaidi kuliko wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kuna hukumu ilio bora zaidi kuliko hukumu yake, basi anakuwa kafiri. Dalili ya hilo ni kwamba hakushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah. Kwa sababu kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah kunapelekea kumsadikisha katika maelezo yake, kutendea kazi na kuhukumiana na Shari´ah Yake. Aidha kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo Yake.

Kwa hiyo yule mwenye kuamini kuwa kuna uongofu bora zaidi kuliko wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kwamba kuna hukumu bora zaidi kuliko hukumu yake, hakushuhudia ya kuwa yeye ni Mtume wa Allaah. Shahaadah yake kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah inabatilika. Atakayeona kuwa kuna uongofu bora kuliko uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), sawasawa na uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ya kwamba kuna hukumu yenye kulingana na hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi amekufuru. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika uongofu bora ni uongofu wa Muhammad.”[1]

Vivyo hivyo ikiwa ataamini kuwa uongofu na hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio kamilifu zaidi, lakini hata hivyo akaona kuwa inafaa kufuata mwongozo wa asiyekuwa Mtume na kwamba inafaa kuhukumiana na isiyokuwa hukumu yake, basi anakuwa kafiri. Kwa sababu atakuwa amehalalisha jambo ambalo kilazima linajulikana uharamu wake.

[1] Muslim (1955) na Ahmad (14689).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 15/04/2023